Jul 01, 2020 12:58 UTC
  • Rais Rouhani: Askari magaidi wa Marekani wanapaswa kuondoka magharibi mwa Asia hususan Syria

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa suala la kuheshimu mamlaka ya Syria na kujitawala nchi hiyo ni msingi mkuu ambao haupaswi kuguswa na kusisitiza kuwa, wanajeshi magaidi wa Marekani wanapaswa kuondoka eneo la magharibi mwa Asia hususan huko Syria haraka iwezekanavyo.

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo alasiri ya leo katika mkutano wake uliofanyika kwa njia ya video na marais Vladimir Putin wa Russia na Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki katika mchakato wa Mazungumzo ya Astana. Amesema, kuwepo kinyume cha sheria wanajeshi vamizi wa Marekani katika ardhi ya Syria kunateteresha amani na utulivu nchini humo na katika eneo zima la magharibi mwa Asia. 

Rais Rouhani amesema kuwa vikwazo vya upande mmoja na vya kikatili vya Marekani dhidi ya Syria vilivyopewa jina la Caesar (Caesar Sanctions) ni njia ya kudumisha jitihada zilizofeli za nchi hiyo za kudhamini maslahi haramu ya kisiasa huko Syria na amesisitiza kuwa: Hatua hiyo ni aina ya ugaidi wa kiuchumi na ukiukaji wa haki za binadamu na mamlaka ya mataifa mengine.

Kikao cha mazungumzo ya Astana

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amelaani hatua yoyote ya kuyawekea vikwazo mataifa mbalimbali duniani hususan taifa la Syria na kusema: Jamhuri ya Kiislamu itaendeleza kwa nguvu zote misaada na uungaji mkono wake kwa watu wa Syria na serikali yao halali, na hatua zinazokiuka sheria na zisizo za kibinadamu za Marekani hazitaweza kuvunja irada na azma ya nchi marafiki na waitifaki wa Syria.

Rouhani ameongeza kuwa, Marekani inapasa kuelewa kuwa, kile ilichoshindwa kukipata kwa kutumia mashinikizo ya kijeshi na kwa kuyasaidia makundi ya kigaidi haitaweza kukipata kupitia mashinikizo ya vikwazo na kuwatesa raia wa kawaida wa Syria. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesisitiza kuwa, mapambano dhidi ya ugaidi yataendelea hadi ugaidi utakapofutwa kabisa nchini Syria na eneo lote la magharibi mwa Asia. 

Tags

Maoni