Jul 02, 2020 02:38 UTC
  • Tishio la Marekani la kutumia chaguo la nguvu za kijeshi dhidi ya Iran; kiwewe cha kushindwa kidiplomasia Washington

Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, Marekani imekuwa na utendaji wa chuki na hasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo ikitumia visingizo tofauti, imetishia mara chungu nzima kutumia mabavu na nguvu za kijeshi dhidi ya Tehran.

Jambo hilo limekuwa likikaririwa na viongozi wa Marekani katika minasaba mbalimbali chini ya anuani ya “chaguo la nguvu za kijeshi lipo mezani”.

Katika fremu hiyo, Brian Hook, mwakilishi maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran hajapinga uwepo wa chaguo la kijeshi dhidi ya miradi ya nyuklia ya amani ya Iran na kwa mara nyingine tena amesisitiza juu ya kuongezwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hook amesema: Sisi bado tunalo mezani chaguo la kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya taasisi za nyuklia za Iran; na Washington inafanya juhudi ili muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran uongezwe. Iran imekuwa ikivuruga amani na uthabiti wa eneo la Asia Magharibi na kama China na Russia zinataka kuweko utulivu katika eneo hilo, basi zinapaswa kuafiki suala la kuongezwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Tehran.

Kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran unafikia tamati tarehe 18 Oktoba mwaka huu. Brian Hook amedai kwamba, kwa sasa Marekani inafadhilisha suala la kuongezwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran na kwamba, filihali haina mpango wa kufuatilia utaratibu wa kusuluhisha mzozano katika JCPOA, unaojulikana kama "Utaratibu wa Kifyatuo", kwa kimombo “Trigger Mechanism.”

Kelly Craft, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa na Brian Hook mwakilishi wa Washington katika masuala ya Iran siku chache zilizopita walitoa ufafanuzi kwa Baraza la Usalama kuhusiana na muswada uliopendekezwa wa kuongezwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran.

Katika mkutano wa Baraza la Usalama uliofanyika kwa njia ya mawasiliano ya Internet usiku wa kuamkia Jumanne iliyopita kwa ajili ya kujadili suala hilo, licha ya madai yaliyotolewa na Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani na ombi lake la kutaka kuongezwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran, lakini Russia na China zilitangaza waziwazi kupinga pendekezo hilo na hata washirika wa Washington barani Ulaya sambamba na kusisitiza ulazima wa kulindwa na kubakishwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA walipinga vikali tishio la Marekani la kutumia utaratibu wa kusuluhisha mzozano katika JCPOA, unaojulikana kama "Utaratibu wa Kifyatuo".

Kwa kuzingatia pigo hilo kubwa ililopata Mrekani, hivi sasa viongozi wa serikali ya Trump wanafikiria kutumia tishio la kijeshi dhidi ya Iran ili kulifanya taifa hili lilegeze msimamo na hivyo kulizuia lisitekeleze mambo ambayo kimsingi ni kwa maslahi yake ya kitaifa hususan katika uga wa tekonolojia ya nyuklia na uwezo wa nyuklia na kuongeza nguvu na uwezo wake wa kiulinzi katika fremu ya kulinda maslahi ya kitaifa na usalama wake wa kitaifa.

Brian Hook, mwakilishi maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran

Kisingi ni kuwa, Marekani licha ya kuendesha propaganda kubwa na kuhaha huku na kule ikifanya mazungumzo na huyu na yule sambamba na kuendesha mashinikizo mtawalia dhidi ya washirika na washindani wake imeshindwa kufikia malengo yake kupitia majukwaa ya kimataifa. Na ndio maana hivi sasa imeamua kurejea kwenye utendaji na mbinu yake kongwe ya chaguo la nguvu za kijeshi dhidi ya miradi ya nyuklia ya Iran ambayo inafanyika kwa malengo ya amani na chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

Pamoja na hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza mara chungu nzima kwamba, tishio lolote lile la kijeshi au uvamizi tarajiwa kutoka kwa Marekani au washirika wake wa kieneo, utakabiliwa na jibu kali. Katika kipindi cha utawala wa Rais Donald Trump mwenendo wa Washington wa kuudhofisha na kuusambaratisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umechukua kasi zaidi.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) liko tayari kukabiliana na chokochoko yoyote ile ya adui

Trump baada ya kutangaza kuiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA alihuisha vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran katika fremu ya siasa za “Mashinikizo ya Kiwango cha Juu Kabisa”. Kwa hatua hiyo Trump akawa ameingia katika vita vya kiuchumi na Iran. Mwaka jana pia Trump akitumia kisingizio cha tishio la Iran dhidi ya majeshi ya Marekani na washirika wake katika Ghuba ya Uajemi aliasisi Muungano wa Baharini na hivyo kuingia katika uga wa vitisho vya kijeshi dhidi ya Iran.

Pamoja na hayo, Iran si tu kwamba, imetoa majibu makali kwa vitisho hivyo vya Marekani, bali imefanikiwa katika nyuga mbalimbali kuongeza nguvu zake za kitaifa. Uwepo wa kijeshi wenye nguvu wa Iran katika Ghuba ya Uajemi sambamba na kuwa na uwezo wa kumfanya adui asithubutu kushambulia hususan katika uga wa uwezo wa makombora ni jambo linaloonyesha kwamba, si tu kwamba, Tehran haina hofu yoyote na vitisho vya Marekani, bali endapo adui atafanya kosa na kufanya uvamizi au shambulio la kijeshi kama vile dhidi ya taasisi zake za nyuklia, basi jibu la Iran dhidi ya Marekani na washirika wake hususan utawala haramu wa Israel litakuwa kali na la kuumiza mno.

Tags

Maoni