Jul 02, 2020 11:38 UTC
  • Mchakato wa Astana; hakikisho la kupatikana amani, utawala huru na mamlaka ya kitaifa ya Syria

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Mchakato wa Astana ungali ndio mpango pekee uliofanikiwa kusaidia kutatua mgogoro wa Syria kwa njia ya amani.

Rais Hassan Rouhani alitoa sisitizo hilo jana Jumatano tarehe Mosi Julai katika kikao cha pande tatu cha "Mchakato wa Astana" kilichofanyika kwa njia ya video na kwa uenyeji wa Tehran, kikishirikisha viongozi wa nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki.

Rais wa Iran aliwahutubu marais Vladimir Putin wa Russia na Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki kwamba: Mchakato wa Astana umekuwa na mafanikio mazuri; kwa hiyo ni jukumu la nchi tatu rafiki na jirani kuulinda na kuuendeleza, zikiwa ndizo wadhamini wa mchakato huo.

Rais Hassan Rouhani akihutubia kikao cha Mchakato wa Astana

Mchakato wa Astana ulianizshwa Januari 2017 kwa ubunifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikishirikiana na Russia na Uturuki; na kutokana na mashauriano ya kila mara ambayo yamekuwa yakifanywa na nchi hizo tatu wadhamini wa mchakato huo, mgogoro wa Syria umeonyesha muelekeo wa kutatuliwa kwa njia ya amani.

Mchakato wa amani wa Astana umeanzishwa nje ya mduara wa matakwa ya Marekani na mtazamo wa Ulaya; na kwa kuzingatia muelekeo na sera za pamoja za Iran, Russia na Uturuki kuhusiana na mgogoro wa Syria na sisitizo lao la kulindwa mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya nchi hiyo, mchakato huo umekuwa chanya na wa mafanikio.

Kutilia mkazo vita dhidi ya ugaidi, kuheshimu matakwa ya wananchi katika kalibu ya mazungumzo ya baina ya Wasyria wenyewe na muhimu zaidi ya yote, kusisitiza kulindwa mamlaka ya ardhi yote ya Syria kupitia mapambano dhidi ya ugaidi, ndio mtazamo wa pamoja wa nchi zinazosimamia Mchakato wa Astana, ambao ufanisi wake umethibitika wazi hivi sasa licha ya kuwepo baadhi ya tofauti za mitazamo.

Kutoka kushoto: Marais Rouhani wa Iran, Putin wa Russia na Erdogan wa Uturuki katika vikao vya Mchakato wa Astana 

Iran inaitakidi kuwa, ijapokuwa kupambana na ugaidi ni mtazamo sahihi katika mgogoro wa Syria, lakini kuheshimiwa mamlaka ya kitaifa na kujitawala kwa nchi hiyo nao pia ni msingi usio na shaka na ambao inapasa uzingatiwe na kupewa umuhimu katika vita dhidi ya makundi ya kigaidi.

Kuna haja ya kutiliwa maanani msingi huu muhimu, kwamba kuwepo Syria moja iliyoungana na inayojitawala bila ya uwepo haramu na usio wa kisheria wa majeshi ya kigeni, si tu kutasaidia kurejesha utulivu nchini humo, lakini pia kutatoa msukumo mkubwa wa kuleta uthabiti na usalama kwa majirani wa nchi hiyo.

Hatu yoyote ya kuyapiga vita makundi ya kigaidi na ya kuondoa wasiwasi wa usalama zilionao nchi jirani na Syria, inahitaji mashauriano na ushirikiano na serikali kuu ya Damascus; na hatua yoyote ile itakayochukuliwa kwa upande mmoja katika suala hilo haitasaidia kupatikana amani na usalama na kuifanya Syria nchi moja iliyoungana.

Mkutano wa Mchakato wa Astana wa amani ya Syria ulipofanyika Januari 2017 katika mji mkuu huo wa Kazakhstan

Nukta ambayo viongozi wa nchi tatu wanachama wa Mchakato wa Astana wamekuwa wakiifanyia kazi katika ushirikiano wao kupitia mchakato huo, ni kutilia mkazo kwa wakati mmoja mapambano dhidi ya ugaidi chini ya usimamizi wa serikali kuu ya Syria na kusisitiza pia ufanisi wa njia ya ufumbuzi kupitia mazungumzo baina ya Wasyria wenyewe sambamba na kulinda mamlaka ya kujitawala ya ardhi yote ya nchi hiyo.

Kuhusiana na suala hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema: Kikao kilichofanyika kwa njia ya video cha viongozi wa nchi wanachama wa Mchakato wa Astana kilikuwa cha mafanikio; na pande husika zimekubaliana kuendeleza ushirikiano baina ya nchi tatu za Mchakato wa Astana kwa kuelekeza juhudi zao katika kupunguza mivutano, kuendeleza mchakato wa kisiasa na utoaji misaada ya huduma za kibinadamu. 

Mashauriano endelevu ya marais wa Iran, Russia na Uturuki yanaonyesha kuwa, mgogoro wa Syria hauwezi kutatuka isipokuwa kwa njia ya kisiasa; na uingiliaji wowote na uwepo wa aina yoyote ile wa majeshi ya kigeni katika nchi hiyo ni kikwazo kwa utekelezaji kamili wa mpango wa mazungumzo baina ya Wasyria wenyewe.../   

Tags

Maoni