Jul 03, 2020 08:11 UTC
  • Marekani yaanzisha chokochoko mpya za kutaka kuzizuia meli za Iran zisipeleke mafuta Venezuela

Baada ya Marekani kushindwa katika chokochoko zake za karibuni za kutaka kuzuia meli za mafuta za Iran zisiingie na kutia nanga katika bandari ya Venezuela, tayari imeshaanzisha chokochoko nyingine mpya za kuzuia muamala halali na wa kisheria wa biashara kati ya nchi hizo mbili.

Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, waendesha mashtaka kadhaa wa serikali kuu ya Marekani jana waliandaa hati ya malalamiko ya kutaka kuzuiwa shehena za mafuta yanayosafirishwa na meli za mafuta za Iran kuelekea Venezuela.

Katika hati yao hiyo ya malalamiko, waendesha mashtaka hao wamewasilisha tuhuma dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Venezuela na kudai kwamba, hivi sasa meli nne za mafuta za Iran zinaelekea Venezuela zikiwa zimebeba jumla ya mapipa milioni 1.1 ya mafuta.

Tarehe 24 ya mwezi uliopita wa Juni, wizara ya fedha ya Marekani ilisisitiza katika taarifa kwamba, inafanya kila njia ili kukwamisha uungaji mkono wa Iran kwa Venezuela na kuongeza kwamba, imewaunganisha kwenye orodha yake ya vikwazo manahodha watano wa meli zilizohusika katika kusafirisha mafuta ya Iran kuelekea Venezuela.

Wafanyakazi wa sekta ya mafuta ya Venezuela wakipongeza na kufurahia meli za mafuta za Iran zilipotia nanga katika bandari za nchi hiyo

Hivi karibuni na katika hatua ya kuisaidia na kuiunga mkono serikali na wananchi wa Venezuela waliowekewa mzingiro wa kiuchumi na Marekani, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilituma nchini humo meli tano za mafuta zilizokuwa zimebeba shehena yenye jumla ya mapipa milioni moja na nusu ya mafuta.

Iran ilituma meli tano hizo za mafuta nchini Venezuela ili kumaliza uhaba wa mafuta katika nchi hiyo ya Amerika ya Kusini licha ya vitisho kadhaa vilivyotolewa na Marekani.

Kufuatia hatua hiyo ya Iran, Rais Nicolas Maduro wa Venezuela aliandika ujumbe katika akaunti yake ya Twitter kuishukuru Jamhuri ya Kiislamu kwa msaada wake kwa serikali na wananchi wa nchi yake na akaeleza kwamba: Venezuela haiko peke yake, bali ina marafiki mashujaa waliosimama nayo bega kwa bega.../

Maoni