Jul 03, 2020 12:04 UTC
  • Kamal Kharrazi
    Kamal Kharrazi

Mkuu wa Baraza la Stratejia za Uhusiano wa Kigeni nchini Iran amesema siasa zisizo sahihi za Marekani na nchi za Ulaya dhidi ya Tehran hazitafua dafu, na kinyume chake, zitapelekea kusambaratika mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Kamal Kharrazi amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitasalimu amri mbele ya sera za kutumia mabavu za nchi za kigeni na kuongeza kuwa, siasa zisizo sahihi za nchi tatu za Ulaya wanachama katika mapato ya nyuklia ya JCPOA (Uingereza, Ufaransa na Ujerumani) zikiongozwa na Marekani kwa ajili ya kusimamisha miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia yenye malengo ya amani ya Iran zimekuwa na matokeo kinyume na matarajio yao, na Tehran imeazimia zaidi kustawisha teknolojia yake ya nyuklia. 

Kharrazi ameashiria mienendo inayotia shaka ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, Rafael Grossi, baada ya kukutana kwake na Mjumbe Maalumu wa Serikali ya Marekani katika Masuala ya Iran, Brian Hook, na kusema: Mkutano na mazungumzo hayo vinaakisi utegemezi na kutokuwa huru mkurugenzi huo wa wakala wa IAEA na kuonyesha ni kutoka wapo Bwana Rafael Grossi anapewa maagizo.

Rafael Grossi na Brian Hook

Mkuu wa Baraza la Stratejia za Uhusiano wa Kigeni nchini Iran amesisitiza kuwa, siasa zisizo sahihi za nchi za Ulaya haziwezi tena kuvumiliwa na Iran na kuongeza kuwa: Hii leo Tehran ina uwezo wa kutengeneza na kusimika kiwango kikubwa cha mashenepewa zenye nguvu kubwa na kuzidisha uwezo wake wa kuzalisha nishati katika kipindi kifupi, kama jibu kwa mienendo ya nchi za Magharibi ya kutotekeleza majukumu yao katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. 

Tags

Maoni