Jul 07, 2020 02:28 UTC
  • Sisitizo la Kiongozi Muadhamu kuhusu Iran kuunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amejibu barua kutoka kwa mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kuhusu matukio ya hivi karibuni ya Palestina.

Katika jibu lake, Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa Iran haitasita kufanya lolote kuwaunga mkono Wapalestina wanaokandamizwa na kuangamiza shari ya utawala bandia na ghasibu wa Kizayuni.

Kiongozi Muadhamu katika barua yake hiyo aliyomuandikia Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ambayo imesambazwa Jumatatu, ameshukuru hatua ambazo zimechukuliwa na harakati za muqawama na mapambano ya Palestina katika kukabiliana na njama za Marekani na utawala wa Kizayuni na kusema hatua hizo zimepelekea umma wa Kiislamu kupata izza na taadhima. Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa: Adui dhalili ambaye amepata vipigo visivyoweza kufidika katika medani ya mapambano, anaendeleza mkakati wake wa kujipanua na kupora haki zisizo na shaka za Wapalestina, aliouanzisha kwanza kwa mashinikizo ya kiuchumi na mzingiro dhidi ya Gaza inayodhulumiwa, na kisha akauendeleza kwa hila na ghilba ya mazungumzo na mpango wa suluhu na mapatano.

Hatima ya taifa la Palestina leo imefika katika awamu nyeti. Katika kipindi hiki cha kihistoria, kuna njama hatari inayotekelezwa ambayo lengo lake ni kuangamiza utambulisho wa Palestina.

Njama hii inatekelezwa katika mchakato wa kile ambacho kimetajwa kuwa ni 'Muamala wa Karne'.

Ushahidi unaonyesha kuwa utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel, kwa msaada wa moja kwa moja wa Marekani, unataka kubadilisha muundo wa kisiasa na kijamii wa ardhi ambazo umezikalia kwa mabavu. Lengo kuu la mpango huo awali kabisa ni kuubadilisha utawala wa Kizayuni kuwa nchi na taifa la Kiyahudi na katika awamu ya pili ni kuwapa Wapalestina mamlaka duni sana katika fremu ya mipaka ya 1967.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei (kulia) na  Ismail Haniya, mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) katika mkutano mjini Tehran miaka iliyopita

Majid Safataj, mtaalamu wa masuala ya Palestina katika uchambuizi kuhusu malengo ya Marekani katika mradi wa 'muamala wa karne' anasema: "Israel inalenga kutumia 'muamala wa karne' kusambaratiisha haki ya wakimbizi Wapalestina kurejea. Kuhusiana na nukta hii, Saudi Arabia inashirikiana na Marekani kutekeleza lengo hilo la Israel kivitendo."

Kuzima shari hii hakuwezekani bila kuendelezwa mapamabano na muqawama. Kimsingi kadhia ya Palestina ni jihadi kubwa ya taifa kwa lengo la kuchukua haki yake ya kihistoria. Ni kwa msingi huo ndio Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika barua yake ya majibu kwa mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas kuhusiana na matukio ya hivi karibuni ya Palestina akasisitiza kuhusu udharura wa kuwa macho na kudumishwa umoja na mshikamano wa wananchi na harakati za Palestina ili kuzima njama chafu za adui. Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa: Kama ilivyokuwa huko nyuma na kwa kuzingatia wajibu wake wa kidini na kiutu na uliosimama juu ya misingi ya thamani za Mapinduzi ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitasita kufanya kila jitihada kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina, kupigania kupatikana haki zao na vilevile kuvunja na kuzima shari ya utawala bandia na ghasibu wa Kizayuni.

Kile ambacho kiko wazi ni kuwa, harakati kubwa ya kihistoria ya muqawama au mapambano ya Palestina imeweza kuendelea kwa muda mrefu kwa mantiki na uzoefu na haijaweza kusambaratishwa kwa vitisho au vishawishi vya maadui. Katika upande wa pili wa harakati hii kubwa ya kihistoria na yenye kuanisha hatima ni ulimwengu wa Kiislamu ambao una jukumu la kujitahidi na kupambana kijihadi kwa ajili ya uhuru na ukombozi wa taifa la Palestina.

Sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kutekeleza kivitendo jukumu hilo kubwa kwa kuunga mkono taifa la Palestina katika hali yoyote ile. Kwa hakika moja ya sababu kuu ambazo zimepelekea madola ya kibeberu yahasimiane na yachukizwe na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kwa sababu nchi hii imeendelea kuunga mkono taifa la Palestina. Ifahamike kuwa uhasama na mashinikizo ya maadui hayataifanya Iran isitishe msimamo wake imara wa kulitetea taifa la Palestina.

Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala bandia wa Israel

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia huko nyuma katika kujibu barua nyingine ya Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina ambaye alikuwa ameandika kulishukuru taifa la Iran kwa uungaji mkono wake kwa taifa la Palestina alisema:"Msimamo daima wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umekuwa ni kuliunga mkono kikamilifu taifa la Palestina."

Irada hii imara bila shaka itakuwa kwa maslahi ya kuliwezesha taifa la Palestina kufikia malengo yake matakatifu. Hii ndiyo nukta ambayo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza katika kujibu barua ya Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hama kuhusu matukio ya hivi karibuni ya Palestina.

 

Tags

Maoni