Jul 07, 2020 09:51 UTC
  • Hotuba ya Zarif katika mkutano wa Jukwaa la Meditereniani; sisitizo la ushirikiano wa kimataifa la kukabiliana na mielekeo ya upande mmoja

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amehutubia katika mkutano wa Jukwaa la Meditereniani (MED 2020) uliofanyika kwa njia ya intanet Jumatatu ya jana tarehe 6 Julai na kusisitiza juu ya kuweko ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na mielekeo ya upande mmoja.

Dakta Muhammad Javad Zarif amebainisha hali inayokabiliwa nayo dunia hii leo na kueleza kwamba, kwa sasa ulimwengu unakabiliwa na virusi viwili, kirusi cha corona na kirusi kingine ni misimamo na mielekeo ya upande mmoja ya Marekani.

Zarif ameongeza kuwa, ulimwengu kwa sasa unakabiliwa na changamoto kubwa mno, kwani uchukuajia maamuzi wa upande mmoja wa Marekani umehatarisha sana misingi ya mahusiano ya kimataifa.  Aidha katika hotuba yake hiyo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria suala la usalama wa eneo la Asia Magharibi na kueleza kwamba, linalonisikitisha mno ni kuwa, sijaweza kuwakinaisha majirani zangu kwamba, tunapaswa kushirikiana kuhusiana na suala la usalama wa eneo.

Mkutano wa Jukwaa la Mazungumzo ya Meditereniani (MED 2020) ni fursa mwafaka kwa ajili ya kubainisha mitazamo na nadharia mbalimbali hususan kuhusiana na masuala ya kieneo na kimataifa. Katika mkutano huo Dakta Zarif amebainisha matokeo mabaya ya uchukuaji maamuzi ya upande mmoja kwa hatima na mustakabali wa mataifa.

Rais Donald Trump wa Marekani

Mkutano huo umefanyika katika hali ambayo, suala la kukabiliana na siasa za upande mmoja za Marekani ni hitajio na dharura ya kimataifa. Jamii ya kimataifa inafanya juhudi ili kuhakikisa kwamba, inapata njia mwafaka ya kukabiliana na siasa hizi na hivyo kuzuia hilo lisije likawa ada na mazoea katika mahusiano ya kimataifa.

Kitovu cha tishio hilo bila shaka ni Marekani. Kuna mfano wa wazi katika uwanja huo nao ni makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ambayo yalifikiwa kwa juhudi za kila upande za nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na madola ya Ulaya na kupelekea kuimarishwa amani na usalama wa kimataifa; lakini Marekani ambayo yenyewe ilikuwa mmoja wa wanachama wa makubaliano hayo, ilijitoa katika makubaliano hayo na hivyo kuthibitisha kwamba, haiafikiani kivyovyote na ushirikiano wa kimataifa.

Katika mkutano huo Dakta Zarif sambamba na kubainisha kwamba, matunda makubwa yaliyopatikana kupitia ushirikiano wa kimataifa ni makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ameeleza pia kwamba: Sisi tumeweza kuipatia ufumbuzi kadhia hii kupitia njia za kidiplomasia kwani ingewezekana kuibuka vita.

Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran

Hata hivyo, hivi sasa kwa mara nyingine tena Marekani imezua mzozo na mgogoro katika mahusiano ya kimataifa kupitia kulirejesha faili la nyuklia la Iran katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa Jana Jumatatu aliashiria harakati za Marekani zilizo dhidi ya makubaliano ya JCPOA na kusema, Marekani imeanzisha mchezo tata. Lengo la Marekani ni kutumia utaratibu wa kusuluhisha mzozano katika JCPOA, unaojulikana kama "Utaratibu wa Kifyatuo", kwa kimombo "Trigger Mechanism" na kuongeza muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran ambapo kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia vikwazo hivyo vinapaswa kuondolewa ifikapo tarehe 18 Oktoba. Serikali ya Donald Trump inafanya juhudi za kila upande ili vikwazo hivyo dhidi ya Iran viwe vya daima.

Kabla ya hapo pia, Marekanii ilifanya juhudi mara kadhaa ili kulirejesha faili la nyuklia la Iran katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini haikufanikiwa. Hityo ilitkana na upinzani wa kimataifa dhidi ya hatua hiyo. Filihali Marekani inafanya njama za kuionyesha Iran kuwa ni tishio kwa usalama wa dunia.  Harakati hizo za Marekani zinafanyika kwa kutoa tuhuma na kupitia Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kupotosha ukweli wa mambo kuhusiana na hatua zilizochukuliwa na Iran za kupunguza majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia baada ya madola ya Ulaya kutotekeleza ahadi zao.

Hii ni katika hali ambayo, hatua zilizochukuliwa na Iran ni majibu kwa  kutowajibika madola ya Ulaya wanachama wa JCPOA na hatua hizi za Tehran si tu kwamba, hazikiuki makubaliano hayo bali ni utekelezaji wa makubaliano yenyewe. Kuhusiana na hilo, Dakta Zarif ametanabahisha kwamba, endapo madola ya Ulaya yataanza kutekeleza kile kilichofikiwa makubaliano, basi itawezekana kuyakoa makubaliano hayo ya JCPOA.

Ni jambo lililowazi kwamba, sera za Iran za kukabiliana na siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa ya Marekani ni kusimama kidete kwa kiwango cha juu kabisa ambapo taifa la Iran likiwa na historia ya maelfu ya miaka katu halitasalimu amri mbele ya mabavu, mabeberu na ukwepaji sharia. Kile ambacho kwa sasa kulingana na mazingira maalumu yaliyopo kwa jamii ya kimataifa ni hitajio muhimu mno, ni kuimarisha mwenendo wa mazungumzo kwa ajili ya amani na usalama, ushirikiano wa kiuchumi, kuandaliwa mazingira kwa ajili ya kufanyika kazi za pamoja na kubwa zaidi ni kustafidi na tajiriba za pamoja kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 ambao kwa sasa ndilo tatizo kuu lililoukumba ulimwengu.

Maoni