Jul 07, 2020 11:06 UTC
  • Zaidi ya watu laki mbili wapata afueni ya corona nchini Iran

Msemaji wa Wizara ya Afya ya Iran ametangaza kuwa, hadi hivi sasa waathirika laki mbili na saba wa ugonjwa wa COVID-19 au corona humu nchini wamepata afueni na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini na katika vituo vya afya.

Bi. Sima Sadat Lari, Msemaji wa Wizara ya Afya ya Iran ametangaza hayo leo Jumanne katika kikao cha kila siku na waandishi habari na kuongeza kuwa, wagonjwa wapya 2,637 wa COVID-19 wamegunduliwa nchini  Iran katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita kufikia leo adhuhuri. 

Bi. Sadat Lari amesema baina ya kesi mpya za maambukizi zilizoripotiwa, 1,455 wamelazwa hospitalini na waliosalia wamepata matibabu bila kulazwa na kwamba kwa ujumla watu walioambukizwa COVID-19 nchini Iran hadi leo mchana ni 245,688.

Wagonjwa wa corona wazidi kupata afueni nchini Iran

 

Hali kadhalika ameashiria kufariki dunia wagonjwa 200  wa corona humu nchini katika kipindi cha masaa 24 hadi kufikia leo mchana na kusema kuwa, hadi sasa watu 11,931  wameshaaga dunia kwa COVID-19 hapa nchini.

Idadi jumla ya walioambukizwa COVID-19 duniani hadi kufikia Jumanne mchana ilikuwa takriban milioni 11 na laki saba na 68,373 na waliopoteza maisha hadi leo mchana ilikuwa ni zaidi ya watu 541,482 kote ulimwenguni.

Marekani inaongoza duniani kwa maambukizi na vifo vya corona ambapo hadi kufikia leo watu zaidi ya milioni tatu na 41,129 walikuwa wameambukizwa COVID-19 na wengine wasiopungua 132,993 walikuwa wamepoteza maisha nchini Marekani pekee. 

Tags

Maoni