Jul 13, 2020 03:40 UTC
  • Iran yakanusha uvumi wa kuiuzia China kisiwa

Iran imekanusha uvumi kuwa imeiuzia China kisiwa chake cha Kish katika Ghuba ya Uajemi na hali kadhalika imekanusha madai kuwa imeafiki kuiuzia China mafuta ghafi ya petroli kwa bei rahisi.

Abolfazl Amoui, Msemaji wa Tume ya Usalama wa Tiafa na Sera za Kigeni katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, amemnukulu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif akikanusha kuwepo mapatano kama hayo na China.

Akizungumza Jumapili, Amoui amesema Zarif amefanya mazungumzo na tume hiyo ambapo amewasilisha maelezo kuhusu masuala mbali mbali yaliyovuma katika vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na kikao cha Bodi ya Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa NIshati ya Atomiki na pia mapatano baina ya Iran na China.

Amoui, Msemaji wa Tume ya Usalama wa Tiafa na Sera za Kigeni katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, amesema Zarif ametoa maelezo kuhusu rasimu ya mapatano ya ushirikiano wa miaka 25 baina ya Iran na China na kusema uhusiano wa nchi hizo mbili umejengeka katika msingi wa maslahi ya pamoja na kuheshimiana.

Rais wa China Xi Jinping (kushoto) akizungumza na Rais Hassan Rouhani mjini Tehran, Iran, Jan. 23, 2016. 

Zarif amewafahamisha wanachama wa tume hiyo kuwa, mchakato wa kutayarisha mapatano hayo ulianza wakati rais Xi Jinping wa China alipoitembelea Iran mwaka 2016 wakati nchi mbili ziliamua kuhusu ulazima wa kuwepo mtazamo wa muda mrefu wa uhusiano na kwamba utayarishaji wa mapatano hayo ungali unaendelea.

 

Tags

Maoni