Aug 02, 2020 10:39 UTC
  • Utawala wa Marekani unapaswa kutoa majibu ya uungaji mkono wake kwa makundi ya kigaidi

Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran ilitangaza Jumamosi ya jana tarehe Mosi Agosti kwamba, Jamshid Sharmahd, kiongozi wa kundi la kigaidi la Tondar ambaye alikuwa akiongoza kutoka Marekani operesheni za utumiaji silaha na za uharibifu dhidi ya Iran ametiwa mbaroni na vikosi vya usalama vya taifa hili katika operesheni tata na makini.

Kundi la kigaidi la Tondar liliasisiwa mwaka 2004 na mtu aliyejulikana kwa jina la Fat’hollah Manouchehri anayejulikana kwa lakabu ya Faroud Fouladvand. Gaidi huyo alitangaza lengo la kuasisi kundi hilo kuwa ni kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha mwaka mmoja. Kanali adui ya Televisheni ya Your TV inayomilikiwa na Faroud Fouladvand ndiyo yenye jukumu la kueneza propaganda na kutangaza misimamo ya kundi hilo la kigaidi. Kundi la kigaidi la Tondar mwaka 2008 lilipanga na kutekeleza mlipuko wa bomu katika Huseiniya ya Sayyid Shuhadaa mjini Shiraz katika mkoa wa Fars kusini mwa Iran. Watu 14 wasio na hatia waliuawa shahidi katika shambulio hilo la kigaidi na watu wengine 215 waliokuwa wamekusanyika katika Husseiniya hiyo kwa ajili ya maombolezo ya Imam Hussein (as) walijeruhiwa.

Aidha katika miaka ya hivi karibuni, kundi hilo la kigaidi lilikusudia kufanya operesheni kadhaa kubwa za kigaidi  kama kulipua Bwawa na Sivand Shiraz, kutekeleza milipuko mtawalia katika maonyesho ya vitabu mjini Tehran na kutega na kulipua bomu katika Haram ya Imam Ruhullah Khomeini (MA), lakini kuwa macho na makini vikosi vya usalama vya Iran kulizuia na kusambaratisha njama hizo chafu.

Sayyid Mahmoud Alavi, Waziri wa Usalama wa Taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Marekani imewapa hifadhi katika ardhi yake na hata kuwasaidia kwa hali na mali watu ambao utambulisho wao wa kigaidi unafahamika na mikono yao imetapakaa damu kutokana na kufanya mauaji dhidi ya raia wa Iran wasio na hatia. Himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa makundi kama hayo kunaibua maswali mawili ya kimsingi ambayo kila mtu mwenye insafu na dhamira safi anajiuliza maswali hayo.

Swali la Kwanza: Marekani inawezaje kudai kwamba, inapambana na ugaidi huku ikiwa na faili kama hili?

Swali la Pili: Marekani inazungumzia amani na usalama upi wa Asia Magharibi?

Katika kujibu swali la kwanza tunapaswa kusema kuwa, katika kalibu ya sera eti za kupambana na ugaidi, daima Marekani imekuwa ikipotosha ukweli wa mambo na katika matamshi yake ya ukwamishaji mambo na kuituhumu Iran kwamba, inahatarisha amani na usalama wa eneo,  inafanya hima ya kuonyesha kuwa, ina nafasi chanya katika eneo huku ukweli ukiwa ni kinyume kabisa, kwani walimwengu wanatambua nafasi hasi na harifu ya Washington katika eneo hili.

Kundi la kigaidi la Munafiqin (MKO) limekuwa likiungwa mkono na Marekani

Katika kujibu swali la pili inatupasa kusema kwamba, kile ambacho kinadaiwa na Marekani kwa anuani ya usalama wa Asia Magharibi, kimsingi ni kuhatarisha usalama wa eneo hili kutokana na kuwalea magaidi na kutumia makundi ya kigaidi kama wenzo wa kufikia malengo yake machafu. Kuanzisha mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda na kundi la kigaidi la Daesh ni mfano hai kabisa wa lengo hilo.

Katika utendaji wa serikali ya Marekani wa kuwaunga mkono magaidi tunashuhudia wazi himaya yake kwa harakati za Kundi la Kigaidi na Munafiqin (MKO), yaani lile lile kundi ambalo limekiri kuhusika na operesheni nyingi za kigaidi nchini Iran. Zaidi ya wahanga 17,000 wa ugaidi nchini Iran ni natija ya uungaji mkono kama huu. Kundi la kigaidi lililokuwa likiongozwa na Abdul-Mlaik Rigi, ni moja ya makundi mengine ya kigaidi yaliyotambulika ambayo yanaungwa mkono na Marekani na jukumu lao ni kuhatarisha na kuvuruga usalama wa mashariki mwa Iran.

Abdul-Malik Rigi naye alitiwa mbaroni na vikosi vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika operesheni iliyokuwa na umahiri mkubwa na baada ya kupandishwa kizimbani alihukumiwa kunyongwa.

Gaidi Abdul-Malik Rigi kiongozi wa kundi la kigaidi la Jundullah alipotiwa mbaroni kabla ya kunyongwa baadaye

Marekani mbali na kuyatumia makundi ya kigaidi yanayotenda jinai kama wenzo wa kufikia malengo yake, Januari 3 mwaka huu, ilishiriki yenyewe moja kwa moja katika operesheni ya kigaidi kwa kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassim Suleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mpainduzi ya Kiislamu (SEPAH), ambaye alikuwa ameelekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa serikali ya Baghdad.

Ni kwa kuzingatia kuwa na faili kama hilo, ndio maana Sayyid Abbas Mousavi, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akasisitiza kwamba, Marekani inapswa kutoa majibu ya kueleweka kwa walimwengu kutokana na himaya na uungaji mkono wake kwa kundi la kigaidi la Tondar na makundi mengine ya kigaidi ambayo yanaongoza operesheni zao kutoka ndani ya ardhi ya Marekani na kufanya mauaji ya umwagaji damu dhidi ya raia wa Iran.

Maoni