Aug 03, 2020 08:32 UTC
  • Sisitizo la Iran na Russia la kuimarisha uhusiano wao kufikia kiwango cha uhusiano wa kistratijia

Leonid Slutsky, Mkuu wa Kamati ya Uhusiano wa Kigeni ya Bunge la Russia, Duma, ambaye amefanya safari rasmi ya kikazi mjini Tehran amekutana na kufanya mazungumzo na Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu masuala ya pande mbili.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jana Jumapili, viongozi hao mbali na kuzungumzia masuala ya pande mbili pia waligusia masuala yanayohusiana na mapatano ya kimataifa ya nyuklia mashuhuri kama JCPOA, matukio ya Syria, Iraq, Yemen, Libya na vilevile ushirikiano wa Tehran na Moscow katika michakato ya kieneo na kimataifa.

Moja ya masuala yaliyotiliwa mkazo na Slutsky katika mazungumzo yake mjini Tehran ni udharura wa kuimarishwa ushirikiano wa Iran na Russia katika kubuni mpango wa ushirikiano wa kistratijia wa nchi mbili.

Kuimarishwa ushirikiano wa aina hiyo kwa ajili ya kulinda maslahi makuu ya nchi mbili ni jambo lenye umuhimu mkubwa kwa kutilia maanani kwamba hivi sasa Marekani inafanya juhudi kubwa za kuzuia kuwepo ushirikiano wa namna hiyo, na hasa kutaka kuzuia mwenendo wa kuimarishwa ushirikiano wa Iran na nchi za eneo. Katika uwanja huo, Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza juu ya umuhimu wa kuboreshwa na kusasishwa hati ya ushirikiano wa muda mrefu wa Iran na Russia na kufikishwa katika kiwango cha uhusiano wa kistratijia.

Rais Vladimir Putin wa Russia (kushoto) na Hassan Rouhani wa Iran

Kassim Jalali, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Russia amezungumzia umuhimu wa hati hiyo na kusema: Kiwango cha uhusiano na ushirikiano wa hivi sasa kati ya Iran na Russia ni mkubwa kuliko ushirikiano uliokuwepo katika miongo iliyopita. Hii ni kusema kuwa katika mazingira ya sasa ushirikiano wa pande mbili ni mkubwa na wenye umuhimu zaidi, hivyo nchi hizi zinapasa kuutumia kujinufaisha kupitia mpango jumuishi wa ushirikiano.

Inakaribia miongo miwili sasa tokea itiwe saini 'Hati ya Uhusiano wa Pande Mbili na Misingi ya Ushirikiano wa Nchi Mbili' hapo mwezi Machi 2001. Kwa kutilia maana matukio na mabadiliko yaliyotokea katika ngazi za kimataifa na kieneo, matumaini ya kunufaika na ushirikiano wa nchi mbili za Iran na Russia pia yameongezeka. Kwa ibara nyingine ni kwamba ushirikiano wa pande mbili umeimarika na kuongezeka pakubwa katika miaka kadhaa iliyopita. Mazingira ya sasa katika eneo pia yanazilazimu nchi mbili hizi zibuni mpango kabambe na jumuishi wa kushirikiana kistratijia. Kuanzishwa uhusiano wa kistartijia kati ya Iran na nchi kubwa na muhimu za Asia na  hasa China na Russia ni mjadala ulioanza kujadiliwa yapata muongo mmoja uliopita.

Jarida la Diplomat linaashiria uhusiano unaoendelea kuimarika kati ya nchi tatu za Iran, Russia na China na kuandika: Katika hali ambayo barani Asia uzingatiaji mkubwa umeelekezwa kwenye matukio ya Marekani na washirika wake, lakini wakati huohuo kuna mwenendo mwingine unaoendelea ambapo Russia, China na Iran zimeanzisha uhusiano muhimu kati yazo.

Nchi tatu za Russia, Iran na China zinaandamwa na siasa za upande mmoja za Marekani

Umuhimu wa suala hilo unaonekana wazi katika msimamo wa pamoja wa Iran na Russia. Tunaweza kuashiria katika uwanja huo taarifa iliyotolewa karibuni katika mazungumzo ya Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na waziri mwenzake Sergey Lavrov wa Russia mjini Moscow. Sehemu ya taarifa hiyo inasema: Tehran na Moscow zimeazimia kutekeleza vilivyo misimamo ya pamoja na ya pande kadhaa ambayo imesimama juu ya misingi ya uadilifu na kanuni zinazotambulika kimataifa kwa ajili ya kutatua haraka masuala kieneo na kimataifa.

Kwa mtazamo huo, uhusiano wa kistratijia wa Iran na Russia mbali na kuimarisha uhusiano wa pande mbili, unaweza pia kukabiliana na vitisho vya pamoja vya kieneo vya nchi mbili hizi na hasa siasa za upande mmoja za Marekani, hasa ikitiliwa maanani kwamba Iran na Russia zimethibitisha kivitendo kwamba zina uwezo mkubwa wa kushirikiana kwa ajili ya kutatua haraka na masuala ya kieneo.

 

 

Maoni