Aug 05, 2020 10:46 UTC
  • Rais Rouhani: Iran inaongoza kwa demokrasia kieneo

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria uchaguzi huru wa rais, bunge na asasi zingine za utawala katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unaofanyika moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja na kusema: "Iran inaongoza kwa demokrasia katika eneo."

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo katika kikao cha baraza la mawaziri leo Jumatano na kuashiria mapinduzi ya kikatiba nchini Iran miaka 114 iliyopita na kusema: "Kabla ya nchi yoyote kuwa na bunge, masanduku ya kupigia kura na uchaguzi, mwaka 1906 nchini Iran amri ya katiba ilitangazwa na bunge likaanza kazi zake wakati huo."

Rais Rouhani amesisitiza kuwa, kutokana na ushiriki wa wananchi katika nyuga zote, hakuna dola lolote linaloweza kutoa pigo kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ameongeza kuwa, wakati nchini Iran kuna serikali, bunge na asasi zingine za utawala ambazo huchaguliwa moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa kura za wananchi, hakuna maana kwa mtu aliye katika Ikulu ya White House katika upande mwingine wa dunia kutoa maamuzi kuhusu kuangusha utawala wa wananchi na kuibua ghasia.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema mihimili mitatu ya dola nchini Iran itashirikiana katika kutatua matatizo ya wananchi. Amesema watu wa Iran hawatasalimu amri mbele ya vikwazo visivyo vya kisheria vya maadui na litaendelea na muqawama hadi kufikiwa ushindi.

Marais Hassan Rouhani wa Iran na Michel Aoun wa Lebanon

Wakati huo huo Rais Rouhani amesema Iran iko tayari kutuma misaada ya dharura Lebanon kufuatia mlipuko uliojiri jana mjini Beirut na kuua watu zaidi ya mia moja na kuepeleka wengine wasiopungua 4000 kujeruhiwa.

Rais wa Iran amemtumia ujumbe wa rambi rambi mwenzake wa Lebanon Michel Aoun na kusema Iran iko tayari kutuma misaada ya dawa, kitiba na misaada mingine inayohitajika katika nchi hiyo.

 

Tags

Maoni