Aug 10, 2020 12:31 UTC
  • Sayyid Abbas Mousavi
    Sayyid Abbas Mousavi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amezungumzia juhudi zinazofanywa na Marekani kwa ajili ya kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa: Wamarekani wanatumia vibaya taasisi za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Sayyid Abbas Mousavi ameyasdema hayo leo mjini Tehran katika mkutano wake na waandishi wa habari akizungumzia muswada uliowasilishwa na Marekani kwa ajili ya kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Iran katika Baraza la Usalama. Ameongeza kuwa, kabla ya kuwa dhidi ya Iran, hatua hiyo inakiuka taratibu wa kimataifa na Baraza la Usalama lenyewe. 

Mousavi amesema kuwa Wamarekani wanataka kuliangamiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa au kulidhibiti kikamilifu na kuongeza kuwa, wanachama wa baraza hilo wanapaswa kuwa macho ili wasitumbukie katika mtego wa Wamarekani.

Kuhusu nafasi ya Saudi Arabia katika barua iliyoandikwa na kusainiwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (GCC), na kutumwa Baraza la Usalama akitaka kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema taarifa za kuaminika zinaonesha kuwa, baadhi ya nchi wanachama katika GCC hazijui kilichokuwemo katika barua hiyo.

Sayyid Abbas Mousavi

Mousavi ameashiria pendekezo lililotolewa na Iran kwa ajili ya kuwepo ushirikiano na nchi za Kiarabu za kandokando ya Ghuba ya Uajemi na akasema: "Tunaziambia nchi zinazosema kuwa zina wasiwasi kuhusu suala la kufutwa vikwazo vya silaha kwamba, nyinyi wenyewe mumelifanya eneo la Ghuba ya Uajemi kuwa ghala kubwa la silaha na zana za kijeshi na hatua yenu ya kutuma barua Baraza la Usalama imechukuliwa kwa ajili ya kujipendekeza kwa Marekani." 

Kuhusu madai yaliyotolewa na maafisa wa serikali ya Mrekani kwamba Tehran inaingilia uchaguzi wa rais wa Marekani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, haya ni miongoni mwa madai ya kuchekesha ya Marekani, kwa sababu Iran haijali wala haitilii maanani watu, mirengo na vyama vya ndani ya Marekani, lakini inazingatia sana mienendo, vitendo na miamala yao na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Maoni