Aug 12, 2020 10:32 UTC
  • Vikwazo visivyo vya kisheria haviwezi kulemaza sekta ya ulinzi ya Iran

Wataalamu vijana wa Kiirani hawataruhusu vikwazo visivyo vya kisheria kulemaza vifaa na zana za kijeshi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Akisisitiza suala hilo siku ya Jamanne, Meja Jenerali Nuzar Ni'mati Naibu Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria umuhimu wa nchi kujitosheleza katika sekta ya utengenezaji zana muhimu za kijeshi na kuongeza kuwa wataalamu wa humu nchini wameweza kutengeneza silaha na zana kubwa za kijeshi yakiwemo magari ya kubeba vifaru na makombora ya kijeshi na hivyo kuvunja siasa za madola ya Magharibi za kuhodhi teknolojia ya utenegenezaji wa zana hizo.

Katika miaka michache iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshuhudia ustawi mkubwa katika sekta ya utengenezaji wa zana za ulinzi. Bila shaka msingi wa ustawi huo ni kutegemea uwezo wa ndani ya nchi na kubadilisha vitisho kuwa fursa.

Uzoefu wa miaka 41 iliyopita unathibitisha wazi kwamba nchi za Magharibi si tu kwamba hazina hamu ya kuhamishia elimu na teknolojia zao katika nchi kama Iran bali zimekuwa zikifanya kila juhudi ili kuzuia kufikishwa mafanikio ya kielimu na kiteknolojia nchini Iran. Vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia vinatekelezwa kwa mtazamo huo. Katika upande wa pili, kuna irada na nia thabiti ya kutaka kuvunja siasa hizo za kuhodhi maendeleo ya kielimu, zinazotekelezwa na nchi za Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Droni ya Marekani aina ya Global Hawk iliyotunguliwa na jeshi la Iran

Kuna nukta mbili muhimu zinazopaswa kuzingatiwa kuhusiana na suala zima la ulinzi. Nukta ya kwanza ni kuwa, nchi za Magharibi zinasisitiza juu ya vikwazo na mashinikizo ya juu kabisa kwa lengo la kuidhoofisha Iran katika hali ambayo mfumo huo huo wa ubeberu unashinikiza na kusisitiza juu ya kuuziwa silaha nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi. Bila shaka lengo la siasa hizo linajulikana wazi. Ni wazi kuwa watengenezaji wakubwa wa silaha zinazouzwa ulimwenguni ni mashirika ya nchi za Magharibi, yanayopata faida kubwa kutokana na mauzo ya silaha. Kila mwaka masharika hayo na hasa ya Marekani, hutumia mabilioni ya dola kwa lengo la kufanya utafiti wa kijeshi na kiusalama ili kuzalisha silaha mpya zinazoyadhaminia faida kubwa kila mwaka.

Nukta ya pili ni kuwa kuna udharura wa kuimarisha nguvu za kiulinzi za kitaifa mkabala na maadui wa dhahiri na wasio wa dhahiri ambao daima wanapanga njama za kutoa pigo dhidi ya Iran. Uzoefu unathibitisha katika uwanja huu kwamba kila wakati nchi inapokuwa dhaifu kiulinzi huwapa maadui fursa ya kuishambulia wakati wowote wanaotaka.

Licha ya machungu yote, lakini ni wazi kuwa vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu viliipa nchi hii somo muhimu ikiwa ni pamoja na umuhimu wa kujiamini na kujitegemea katika nyanja tofauti. Katika kipindi hicho pia Iran iliwekewa vikwazo na mabeberu wa kimataifa. Tokea wakati huo juhudi kubwa zilifanyika kwa shabaha ya kujitosheleza katika uundaji wa silaha na hatimaye kuiwezesha nchi kujitosheleza katika uwanja huo.

Hii leo Iran ni moja ya nchi muhimu duniani zinazotengeneza makombora ya kisasa. Mwezi Januari mwaka huu Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, lilijibu kishujaa jinai iliyotekelezwa na Marekani katika kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani ambaye alikuwa amealikwa rasmi na viongozi wa Iraq kuitembelea nchi hiyo. Jeshi hilo lilivurumisha makombora 13 ya balestiki katika kituo kikubwa zaidi cha kijeshi cha Marekani nchini Iraq na hivyo kuthibitisha kivitendo kwamba uchokozi wowote wa adui hautapita bila jibu na kwamba iwapo nchi yoyote itafanya upumbavu wa kuhatarisha maslahi ya Iran bila shaka itakabiliwa na jibu kali la majuto kutoka Iran.

Satalaiti ya kijeshi ya Nur ikirushwa katika anga za mbali

Iran vilevile tarehe 22 Aprili iliyopita iliweza kutuma satalaiti yake ya kwanza ya kijeshi inayoitwa Nur katika anga za mbali kwa kutumia kombora lake linaloitwa Qased.

Fabian Hines mtaalamu katika Kituo cha James Martin anasema ifuatavyo kuhusiana na kurushwa katika anga za mbali satalaiti hiyo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran: 'Huu ni mpango wa hali ya juu na wenye teknolojia ya hali ya juu kabisa na wakitaka wanaweza kuiimarisha na kwenda mbali zaidi.'

Wataalamu wa Kiirani wamewashangaza walimwengu mara nyingi katika kipindi cha kuwekewa vikwazo vikali zaidi duniani na bila shaka wataendelea kuwashangaza siku zijazo na kuwafanya wakiri juu ya uwezo mkubwa wa taifa kubwa la Iran.

Maoni