Aug 12, 2020 10:46 UTC
  • Rouhani: Uwezo wa kijeshi wa Iran ni kwa maslahi ya eneo lote

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inatumia silaha na zana zake kwa ajili ya kulinda nchi mbele ya wavamizi ajinabi na kuongeza kuwa: "Uwezo wa kujihami na kisilaha wa Iran ni kwa maslahi ya eneo lote."

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo Jumatano katika kikao cha baraza la mawaziri na kuongeza kuwa, nchi jirani zinapaswa kuwa macho ili Marekani isizitumie vibaya na kuongeza kuwa: "Nchi za eneo zinapaswa kuchukua tahadhari ili utajiri wa mataifa yao usiporwe na zikabiliane na uuzaji silaha ambao unatumiwa kudondosha mabaomu dhidi ya majirani."

Rais Rouhani amesema Iran ni nchi ya kwanza ambayo ililaani hujuma ya Saddam, dikteta aliyepinduliwa wa utawala wa Baath wa Iraq dhidi ya Kuwait na kuongeza kuwa: "Iran imeonyesha kivitendo kuwa inataka uthabiti katika eneo na iwapo Saddam angeruhusiwa basi dikteta huyo baada ya Kuwait, angevamia na kukalia kwa mabavu Saudia, Qatar na Imarati."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezihutubu baadhi ya nchi za eneo kwa kusema: "Iwapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haingesimama kidete kwa ajili ya uthabiti wa eneo basi baadhi ya nchi jirani zilizo kusini mwa Iran hazingekuwepo."

Rouhani ameashiria rasimu ya azimio la Marekani dhidi ya Iran katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema kupitishwa azimio hilo kutakuwa ni ukiukwaji wa wazi wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA na watakaoliunga mkono watabebe dhima ya matokeo mabaya yatakayofuata. Ameongeza kuwa: "Washington itashindwa mkabala wa Tehran na Iran itapata ushindi katika hatua zake ambazo inachukua kwa mujibu wa sheria na maslahi ya kitaifa."

Rais wa Iran amesema pia hakuna anayepaswa kutumia vibaya tukio la mlipuko wa Beirut Lebanon. Aidha amesema Iran imetuma misaada ya dawa na vifaa vya kitiba nchini Lebanon na kuongeza kuwa watu wa Lebanon watavuka kipindi hiki kigumu kwa mafanikio.

Tags

Maoni