Aug 12, 2020 10:51 UTC
  • Zarif: Marekani haina uwezo wa kutumia mfumo wa kurejesha vikwazo dhidi ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema muswada ambalo Marekani imemependekeza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halitaidhinishwa na baraza hilo na kuongeza kuwa: "Kwa mtazamo wa kisheria, Marekani haina uwezo wa kutumia mfumo wa kurejesha vikwazo dhidi ya Iran."

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Tehran Zarif amesema: "Waitifaki watatu wa Marekani barani Ulaya waliwahi kusema katika kikao kilichopita cha Baraza la Usalama kuwa Marekani haiwezi kutumia mfumo wa Snapback (wa kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran)."

Zarif amezungumza na waandishi habari baada ya Marekani kuwasilisha muswada katika Baraza la Usalama dhidi ya Iran. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Marekani imefanya juu chini kuishawishi dunia irejeshe vikwazo vya silaha dhidi ya Iran lakini imefeli katika jitihada hizo. Amesema Wamarekani wamebaini kuwa muswada wao utapata chini ya kura tano katika Baraza la Usalama lenye wanachama 15 na kuongeza kuwa gazeti la New York Times limetabiri Marekani itapata kura moja au mbili jambo ambalo linaashiria kutengwa Washington kimataifa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Wiki iliyopita Marekani ilikuwa imewasilisha muswada wenye kurasa 13 kuhusu kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran lakini muswada huo imepingwa vikali na wanachama wa Baraza la Usalama na hivyo ikalazimika kuipunguza hadi kurasa nne jana.

Marekani imeanzisha kampeni kubwa za kimataifa za kulizuia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litekeleze azimio lake nambari 2231 linalotoa amri ya kuiondolea Iran vikwazo vya silaha ifikapo tarehe 18 Oktoba mwaka huu wa 2020. Marekani inaendesha njama hizo kama sehemu ya kukabiliana na uwezo mkubwa wa kiulinzi na kijeshi wa Iran unaozidi kukua na kuwa imara siku baada ya siku.

Maoni