Aug 13, 2020 03:30 UTC
  • Marekani yalegeza msimamo kuhusu kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran

Juhudi za Marekani za kutaka vikwazo vya silaha dhidi ya Iran virefushwe katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimekabiliwa na changamoto kubwa.

Katika kujaribu kulinda heshima yake mbele ya macho ya walimwengu, sasa Marekani imelegesa msimamo ili angalau ifikie mapatano ya kiwango cha chini kuhusu suala hilo. 

Katika rasimu mpya iliyoiwasilisha kwa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Marekani imefanya marekeboisho kadhaa muhimu katika rasimu hiyo. Washington imetumia maneno mepesi kuwasihi wanachama warefushe vikwazo hivyo hadi pale Baraza la Usalama litakapochukua msimamo tofauti. Rasimu hiyo pia inaondoa udharura wa nchi tofauti kulazimika kutekeleza marufuku ya uuzaji silaha za Iran. Vilevile nchi hazitalazimika tena kusimamisha na kupekua meli zinazobeba bidhaa za Iran. Kwa mujibu wa rasimu hiyo shakhsia na taasisi za Iran likiwemo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu hazitawekewa vikwazo. Rasimu hiyo imendeelea kukariri madai yasiyo na msingi  kuhusu siasa za eneo za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo imedaiwa kwamba kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran kunalenga kulinda amani na usalama wa kimataifa.

Baadhi ya makombora ya Iran yakirushwa angani

Kwa kutilia maanani upinzani wa Russia na China dhidi ya rasimu ya azimio hilo jipya la Marekani ni wazi kuwa azimio hilo halitafika popote. Kuna shaka kubwa iwapo azimio hilo jipya litapitishwa katika Baraza la Usalama kwa kutilia manani kuwa linapasa kuungwa mkono na wanachama wasiopungua 9 wa baraza hilo na lisipingwe kwa kura ya veto ya nchi mbili hizo.

Ni wazi kuwa rasimu ya awali ya azimio hilo imefanyiwa marekebisho muhimu kwa ajili ya kuwashawishi wanachama wa Baraza la Usalama na hasa nchi za Ulaya ziliunge mkono. Na hasa tukitilia maanani kuwa rasimu ya awali ilipingwa vikali na wanachama wa Baraza la Usalama, zikiwemo nchi za Ulaya kwa hoja kuwa haikuwa ya kawaida na kuwa ilikiuka misingi na taratibu za kidiplomasia.

Ili kufikia lengo lake katika uwanja huo, serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani imekuwa ikitoa mashinikizo makubwa kwa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na hivyo kuibua mgogoro mkubwa kati ya wanachama hao kuhusu suala la vikwazo dhidi ya Iran. Katika uwanja huo mtandao wa habari wa Bloomberg wa Marekani umeonya kwamba kutolewa mashinikizo na vitisho dhidi ya Iran kunaweza kuwa na matakeo yasiyotarajiwa. Limesema kushinikizwa washirika wa Marekani yaani Ujerumani na Ufaransa kunaweza kuzipelekea nchi mbili hizo za Ulaya zielekee upande wa Russia na China na mwishowe kutengwa Marekani katika Baraza la Usalama.

Ni wazi kuwa Marekani imelegeza msimamo wake wa hapo awali kuhusiana na kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana pia na upinzani wa Russia na China ambazo ni wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama. Marekani inatambua vyema kuwa hata kama itapata uungaji mkono wa nchi za Ulaya lakini bila ya kuwa na ushirikiano wa China na Russia haiwezi kufika popote katika kurefusha vikwazo vya Iran. Madola mawili hayo makubwa ya dunia yanazichukulia juhudi za serikali ya Trump za kutaka kurefusha vikwazo dhidi ya Iran kuwa zinakiuka wazi azimio la Baraza la Usalama ambalo linataka vikwazo hivyo viondolewe ifikapo tarehe 18 Oktoba mwaka huu.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Hii ni katika hali ambayo iwapo Marekani itafanikiwa kufikia lengo hilo, bila shaka suala hilo litakabiliwa na jibu kali la Iran na kupelekea kusambaratika mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndipo nchi mbili hizo zikasema kuwa hakuna uwezekano wa kupitishwa rasimu ya azimio hilo la Marena katika Baraza la Usalama.

Hata hivyo Marekani imezituhumu nchi mbili hizo kwamba zimepinga rasimu yake ya vikwazo ili ziweza kupata fursa ya kuiuzia Iran silaha zao. Marekani inazungumza ni kana kwamba imesahau kuwa ndiyo inayoziuzia silaha kwa wingi nchi za kusini mwa Ghuba ya Uajemi na hasa Saudia na Imarati. Inadai kuwa mashindano ya silaha yatatokea katika eneo iwapo Iran itaondolewa vikwazo vya silaha huku ikiwa inajua wazi kuwa Iran imekuwa chini ya vikwazo kwa miaka mingi, jambo ambalo limeipelekea kufanya juhudi za kuunda na kujitosheleza kwa silaha za kujilinda na kujitetea mbele ya maadui wake sugu.

Tags