Aug 14, 2020 08:07 UTC
  • Iran: Uhusiano wa kidiplomasia wa Abu Dhabi na Tel Aviv ni ujinga wa kistratijia

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani hatua ya kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE au Imarati) na utawala wa Kizayuni wa Israel na kutaja hatua hiyo kuwa ni ujinga wa kistratijia ambao bila shaka utapelekea kuimarika mhimili wa muqawama na mapambano katika eneo.

Siku ya Alhamisi, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kufikiwa mapatano baina ya Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala haramu wa Israel kuhusu kuanzishwa uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia baina ya pande mbili hizo.

Kufuatia hatua hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa taarifa mapema leo Ijumaa na kusema: "Watu wanaodhulumiwa wa Palestina, na mataifa yote yanayopenda uhuru duniani kamwe hayatasamehe kitendo cha kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu na utendao jinai wa Israel." Taarifa hiyo imesema kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel ni sawa na kuwa mshirika wa jinai za utawala huo.

Aidha taarifa hiyo imesema hakuna shaka kuwa damu iliyomwagwa kidhalimu katika miongo saba ya muqawama na mapambano kwa ajili ya kupigania ukombozi wa ardhi takatifu ya Palestina, inayojumuisha kibla cha kwanza cha Waislamu, hivi karibuni au baadaye itawasakama wale ambao wamesaliti malengo ya taifa la Palestina.

Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni wa Israel (kushoto) na Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan Mrithi wa Ufalme wa Abu Dhabi

Hali kadhalika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema kitendo cha kuaibisha cha UAE cha kuanzisha uhusiano na utawala wa Israel ambao ni utawala bandia, haramu na ulio dhidi ya ubinadamu ni hatari kubwa.

Aidha Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetahadharisha kuhusu uingiliaji wowote wa utawala huo wa Kizayuni katika mlingano wa eneo la Ghuba ya Uajemi na kuongeza kuwa, serikali ya Imarati na serikali zinginezo zinazoiunga mkono katika kadhia hiyo zitabeba dhima ya chochote kitakachotokea kufuatia hatua hiyo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema historia itaonyesha namna kosa hili la kistratijia la utawala wa Kizayuni na usaliti huu wa Imarati kwa taifa la Palestina na Waislamu wote utakavyopelekea kuimarika mhimili wa muqawama na mapambano na kuleta mshikamano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na tawala zinazopinga mabadiliko katika eneo.

Katika taarifa hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa ushauri kwa watawala wanaoishi katika makasri ya vioo ambao wanakiuka haki za Palestina na watu wengine wanaodhulumiwa katika eneo kama Yemen na kusema watawala hao wanapaswa kutafakari kuhusu mustakabali na kutumia busara na kutofanya kosa la kuwaweka maadui mahala pa marafiki.

Tags

Maoni