Aug 30, 2020 07:16 UTC
  • Iran ya Kiislamu yaghariki kwenye dimbwi la huzuni na majonzi ya maombolezo ya Ashura

Kwa kuwadia Ashura, siku ya kupeperushwa bendera za wekundu wa damu za kupigania uhuru na ukombozi, msisimko wa mapenzi ya Imam Hussein AS umetanda katika kila pembe ya Iran ya Kiislamu.

Wananchi Waislamu waombolezaji katika Iran ya Kiislamu, leo wanashiriki kwenye majlisi za maombolezo kukumbuka ushujaa na dhulma waliotendewa mashahidi wa Karbala.

Matabaka tofauti ya wananchi Waislamu wa Iran wakiwemo vijana na wazee, wake kwa waume wanashiriki kwenye maombolezo hayo ya kukumbuka siku aliyouliwa shahidi Imam Hussein AS.

Harakati za waombolezaji wanaobubujikwa na machozi kwa majonzi na huzuni kwa dhulma iliyofanywa na wana wa shetani dhidi ya kizazi bora cha wanadamu, huku wakipaza sauti zao kupinga madhila na udhalili, zimezijaza hamasa na msisimko mkubwa majlisi za maombolezo ya Siku ya Ashura katika kila pembe ya Iran ya Kiislamu.

Waombolezaji wakishiriki katika majlisi za Muharram kwa kuzingatia na kuchunga miongozo ya kiafya

Kutokana na maombolezo ya mwaka huu kufanyika katika mazingira ya maambukizi ya virusi vya corona, waombolezaji wanashiriki katika majlisi za Ashura zinazofanyika katika maeneo ya wazi kwa nidhamu maalumu inayozingatia na kuchunga kikamilifu miongozo ya kiafya.

Katika tukio la Karbala lililojiri katika siku kama ya leo, Imam Hussein AS, Imamu wa Tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia duniani alisisitiza na kueleza bayana kwamba: "Kusudio langu ni kuufichua na kuufedhehesha utawala ulio dhidi ya Uislamu, kuamrisha mema na kukataza mabaya na kukabiliana na dhulma na uonevu."

Mafunzo ya harakati ya Imam Hussein AS yamesambaa na kutanda katika historia na jiografia ya viumbe, wanadamu na ulimwengu mzima na hayawezi katu kuishia kwenye mipaka maalumu.../

Tags