Sep 13, 2020 12:54 UTC
  • Rais Rouhani: Marekani imeshindwa vibaya katika njama zake dhidi ya Iran

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua haribifu za Marekani dhidi ya uchumi wa Iran na kusema kuwa, adui siyo tu kwamba, ameshindwa kufikia malengo yake ya kistratejia, bali amepata pigo lisilo na kifani katika uwanja huo.

Rais Rouhani amesema hayo leo katika hafla ya kuanza mwaka mpya wa masomo kwa vyuo vikuu na vituo vya elimu ya juu hapa nchini na kueleza kwamba, maadui wa taifa la Iran wakiwa na nia ya kufikia malengo yao kuna wakati walikuwa wakiliona Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama uwanja wao wa kujifaragua lakini katika miezi ya hivi karibuni wamechezea vipigo vya kihistoria.

Rais Hassan Rouhani ameashiria masuala kama mpango wa kutaka kuongezwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran na kutaka kutumia utaratibu wa kusuluhisha mzozano katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, unaojulikana kama "Utaratibu wa Kifyatuo", kwa kimombo "Trigger Mechanism" kuwa miongoni mwa ambayo Marekani ilikwama kuyafikia kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Hafla ya kuanza muhula mpya wa masomo kwa vyuo vikuu na vituo vya elimu ya juu iliyofanyika kwa njia ya mawasiliano ya Intaneti

 

Rais wa Iran aidha ameashiria mafanikio ya kisheria ya Jamhuri ya Kiislamu katika Mahakama ya Kimataifa mkabala na Marekani na kusema kuwa, mafanikio ya kisiasa na kisheria ya Tehran iliyoyapata mkabala na Washington hayakuwa ya kawaida. 

Aidha Rais Rouhani ameashiria mafanikio ya kielimu ya vyuo vikuu vya Iran katika medani za kimataifa  na kuyataja mafanikio hayo kuwa ni ya thamani kubwa. Amesema hii leo vyuo vikuu 40 vya Iran vimo katika orodha ya vyuo vikuu bora zaidi duniani na katika upande wa uvumbuzi na uletaji mambo mapya ya kielimu, katika miaka ya hivi karibuni Iran imepanda kutoka nafasi ya 120 na kufikia nafasi ya 65 duniani.

Tags

Maoni