Sep 16, 2020 11:19 UTC
  • Rais Rouhani: Marekani imefeli katika jitihada zake za kutaka kutumia 'Utaratibu wa kifyatuo'

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Marekani imefeli na kushindwa katika juhudi zake za kutaka kutumia utaratibu wa kusuluhisha mzozano katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, unaojulikana kama 'Utaratibu wa Kifyatuo' kwa kimombo "Trigger Mechanism".

Rais Rouhani amesema hayo leo katika kikao na baraza lake la mawaziri ambapo ameashiria juhudi za Marekani za kutaka kutumia 'Utaratibu wa Kifyatuo' na kusema kuwa, utaratibu huo ni kwa ajili ya nchi wanachama wa makubaliano ya JCPOA.

Rais wa Iran amesema kuwa, taifa ambalo liliyataja makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kuwa ni mapatano mabaya zaidi katika historia ya Marekani na likajitoa katika makubaliano hayo ya kimataifa, halina haki ya kuzungumzia na kutoa maoni kuhusiana na 'Utaratibu wa Kifyatuo'.

Dakta Hassan Rouhani amesema kuwa, Mareani inataka kuanzisha njama mpya dhidi ya Jamhuri ya Kiisamu ya Iran na kuongeza kuwa, wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mataifa matatu ya Ulaya yamebainisha wazi kwamba, yanapinga kutumiwa utaratibu huo.

Baadhi ya mawaziri wakiwa katika kikao na Rais Hassan Rouhani

 

Aidha amesema, ukiacha utawala wa Kizayuni wa Israel na nchi nyingine mbili ndogo katika eneo, Marekani haina mtu mwingine ulimwengu.

Rais Rouhani ameashiria pia kuanzishwa uhusiano wa kawaida wa Imarati na Bahrain na utawala wa Kizayuni na kusema kuwa, watawala wa baadhi ya mataifa ya Kiarabu katika Asia Magharibi hawajali malengo ya taifa madhulumu la Palestina.

Rais wa Iran ameonya kuwa, matokeo yote mabaya ya kuanzisha uhusiano na Israel yatakuwa katika dhima na mabega ya mataifa ambayo yameanzisha uhusiano na Wazayuni kinyume kabisa na kanuni na usalama wa eneo hili.

Tags

Maoni