Sep 17, 2020 08:11 UTC
  • Ali Shamkhani
    Ali Shamkhani

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amejibu vitisho vilivyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Iran na kusema: Wanaoamuru na watekelezaji wa mauaji ya wana wa Iran kama diteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein na wengineo, watapelekwa jongomeo.

Ali Shamkhani amesema hayo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Twitter kwa kutumia hashtagi ya "Kisasi Kikali" na kuandika kuwa: "Wiki ya Kujitetea Kutakatifu inaakisi historia ya azma na irada ya kizazi cha Shahidi Qassem Soleimani kwa ajili ya kuwatia adabu madikteta wanaoona njozi na kudhani kwamba, wana nguvu kubwa zaidi mara elfu moja kuliko Iran."

Tarehe 31 mwezi Shahrivar mwaka 1359 (Septemba mwaka 1980) jeshi la dikteta za zamani wa Iraq, Saddam Hussein lilianzisha vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa kutumia aina mbalimbali za silaha. Tarehe 31 Shahrivar kila mwaka Iran huanza kudhimisha Wiki ya Kujitetea Kutakatifu kwa mnasaba wa kukumbusha tukio hilo. 

Hivi majuzi, jarida la POLITICO la nchini Marekani lilinukuu kile kilichodaiwa ni ripoti za intelijensia za Washington pamoja na maafisa wa karibu na serikali ya nchi hiyo wanaodai kwamba, Iran ina mpango wa kutaka kumuua balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini.

Jarida hilo lilinukuu chombo kisichojulikana na kudai kuwa Tehran ilikuwa na mpango wa kumuua balozi Lana J. Marks wa Marekani mjini Pretoria kwa lengo la kulipiza kisasi cha mauaji yaliyofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani.

Baada ya kutolewa madai hayo Rais Donald Trump wa Marekani alisema kuwa hatua yoyote ile itakayochukuliwa dhidi ya maslahi ya Marekani itajibiwa kwa nguvu kubwa zaidi mara elfu moja. 

Donald Trump

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Saeed Khatibzadeh amekanusha tuhuma hizo za kiuadui na zenye malengo maalumu na akawashauri viongozi wa Marekani waache kutumia mbinu hizo zilizopitwa na wakati kwa ajili ya propaganda dhidi ya Iran katika uga wa kimataifa.

Tags

Maoni