Sep 17, 2020 13:16 UTC
  • Gharib Abadi: Shughuli za nyuklia za Iran zina uwazi zaidi kuliko za nchi nyingine zote wanachama wa IAEA

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao mjini Vienna amesema asilimia 22 ya ukaguzi wote uliofanywa duniani na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA imefanyiwa Iran na akaeleza kwamba Tehran ndiyo inayoendesha kwa uwazi zaidi shughuli zake za nyuklia zenye malengo ya amani kuliko nchi zote wanachama wa wakala huo.

Kazem Gharib Abadi ameyasema hayo leo alipohutubia kikao cha msimu cha Bodi ya Magavana wa IAEA, ambapo sambamba na kubainisha misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu ripoti ya ukaguzi ya Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo wa atomiki ameongeza kuwa: Iran imeamua kwa hiari yake kulikubali ombi la IAEA la kuchunguza baadhi ya masuala yanayodhaniwa tu kuwa huenda yatahitaji kufanyiwa ukaguzi.

Gharib Abadi amesema, kiwango cha juu cha ushirikiano unaoshuhudiwa hivi sasa kati ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki hakijafikiwa kwa urahisi, hivyo haifai kuruhusu ushirikiano huo udhoofishwe kwa sababu ya maslahi finyu tu ya kisiasa ya baadhi ya nchi. Ameongeza kuwa: Ili kulinda umoja wa IAEA, nchi zote wanachama zinapaswa kujiepusha kikamilifu na utoaji mashinikizo ya aina yoyote ile dhidi ya wakala huo wa atomiki.

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao mjini Vienna, ameashiria pia mripuko uliotokea hivi karibuni katika kituo cha nyuklia cha Natanz na akaeleza kwamba, tukio hilo lilikuwa hujuma iliyofanywa na maadui dhidi ya sekta ya nyukila ya Iran; hivyo akasisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu inaamini kuwa ni haki yake kulinda vituo vyake vya nyuklia na kujibu vitisho hivyo kwa namna yoyote ile itakayohisi inafaa.

Katika hotuba yake hiyo Kazem Gharib Abadi amezungumzia pia mienendo inayogongana ya nchi wanachama wa IAEA kuhusiana na silaha za nyuklia za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na akaeleza kwamba: Utawala wa Kizayuni ungali ndio tishio linalotia wasiwasi mkubwa zaidi wa kiusalama katika eneo la Asia Magharibi na kwamba utawala huo una aina kadhaa za silaha za mauaji ya halaiki lakini hadi sasa umekataa miito ya mara kwa mara ya Jamii ya Kimataifa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ya kuchunguzwa na kukaguliwa shughuli zake za nyuklia, huku ukiendelea kutoa vitisho na kuwashambulia kijeshi majirani zake.../

Tags

Maoni