Sep 18, 2020 08:09 UTC
  • Waziri Zarif amjibu Pompeo: Hakuna kitu kipya kitakachofanyika Septemba 20

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu matamshi ya hivi karibuni ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo juu ya njama za Washington za kutaka kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran kwa kutumia mchakato unaofahamika kama 'Snapback Mechanism' na kusisitiza kuwa, 'Hakuna kitu maalumu kitakachofanyika Jumapili ya Septemba 20.'

Muhammad Javad Zarif amesema hayo katika ujumbe wake wa mtandao wa Twitter na kufafanua kuwa, Washington haina haki ya kutumia "Snapback Mechanism", ambao ni utaratibu wa kurejesha upya vikwazo ilivyokuwa imewekewa Iran huko nyuma na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa kuwa si mshiriki tena wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Itakumbukwa kuwa, Mei mwaka 2018, Rais Donald Trump alichukua uamuzi wa upande mmoja wa kuitoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Dakta Zarif amemhutubu Pompeo na kumtaka aende asome vipengee vya JCPOA, badala ya kuendelea kudai kuwa vikwazo hivyo vitaanza kutekelezwa tena Jumapili ijayo. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema hata John Bolton, Mshauri wa zamani wa Usalama wa Taifa wa Marekani ambaye alimshawishi Trump aiondoe Washington katika mapatano hayo ya kimataifa, ana ufahamu zaidi kuhusiana na ukweli huo.

Marekani imeshindwa kufanikisha njama yake ya kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Iran kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na njama za kutaka kutekelezwa Utaratibu wa Kurejesha Vikwazo Papo kwa Papo 'Snapback Mechanism'

Zarif amemnukuu Bolton ambaye mwezi uliopita alisisitiza kuwa ni jambo lisiloyumkinika kwa Marekani kuchukua hatua ya upande mmoja na kuvirejesha vikwazo hivyo dhidi ya Iran kwani kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

Bolton alisema kuwa, juhudi zinazofanywa na seikali ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo za kutaka kutekeleza utaratibu wa "Snapback Mechanism" wa kurejeshwa vikwazo vya UN dhidi ya Iran baada ya njama zake za kutaka kurefushwa marufuku ya silaha dhidi ya Iran kufeli ni hatua ya kipumbavu na kijinga.

Tags

Maoni