Sep 19, 2020 11:04 UTC
  • Afrika Kusini yakadhibisha tuhuma za Marekani dhidi ya Iran

Baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, serikali ya Rais Donald Trump ilizidisha mashinikizo ya kiwango cha juu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa shabaha ya eti kulemaza uchumi wa Iran na imekuwa ikitumia kila liwezekanalo kuanzisha vita vya kinafsi na kisaikolojia ikiwa ni pamoja na kutoa vitisho dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Miongoni mwa harakati hizo za kiadui za Marekani ni madai ya karibuni ya Washington kwamba Iran ina mpango wa kumuua balozi wa nchi hiyo huko Afrika Kusini, Lana Marks ili kulipiza kisasi cha mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na jeshi la Marekani dhidi ya aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Luteni Jenerali Qassem Soleimani. Hata hivyo madai hayo yasiyo na msingi yamekadhibishwa na serikali ya Pretoria. Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesema kuwa, madai yaliyotolewa na jarida la POLITICO kwamba Iran ina mpango wa kumuua balozi wa Marekani mjini Pretoria yanastaajabisha na kushangaza. Dakta Naledi Pandor ameongeza kuwa: Marafiki zetu wa Iran kama tulivyo sisi, wameshangazwa sana na madai haya.  Pandor amesema: "Tumestaajabishwa na kitendo cha kutolewa taarifa kama hiyo kwa umma. Imetushangaza namna ilivyowashangaza pia mafariki zetu nchini Iran." Waziri wa Ushirikiano na Uhusiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini amehoji, "inawezekanaje Iran, rafiki mkubwa wa Afrika Kusini aje hapa nchini na kufanya kitendo kiovu kama hicho katika nchi ambayo pia rafiki yake? Naweza kusema kuwa madai hayo ni ya kushangaza."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Dr Naledi Pandor  

Hivi majuzi, jarida la POLITICO la nchini Marekani lilinukuu kile kilichodaiwa ni ripoti za intelijensia za Washington na kudai kwamba, Iran ina mpango wa kutaka kumuua balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini, Lana Marks. Madai ya jarida hilo yalikaririwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo. 

Muda mfupi baadaye Rais Donald Trump aliparamia mawimbi na kutumia madai hayo kutoa vitisho dhidi ya Iran. Trump ambaye umaarufu wake unaendelea kuporomoka kati ya Wamarekani kabla ya uchaguzi wa rais wa mwishoni mwa mwaka huu, alitoa vitisho visivyo vya kawaida kwenye mtandao wa Twitter na kuandika kwamba: "Shambulizi lolote dhidi ya Marekani kwa sura yoyote litakabiliwa na shambulizi dhidi ya Iran ambalo litakuwa shadidi mara elfu moja zaidi." Mienendo isiyo na mantiki ya serikali ya Rais huyu wa Marekani inashangaza sana hasa tunapozingatia kwamba, ameamua kutoa vitisho dhidi ya Iran kwa kutegemea tu ripoti ya jarida la Kimarekani bila ya kuwa na ushahidi wala waraka wowote wa kuthibitisha madai hayo.

Rais Donald Trump wa Marekani  

Nukta nyingine iliyoshuhudiwa katika ujumbe wa Twitter wa Trump ambayo inapaswa kusajiliwa katika orodha ndefu ya payukapayuka nyingi za kiongozi huyo wa Marekanini ni pale alipokiri kwa kusema kwamba, "kwa mujibu wa ripoti ya vyombo vya habari", Iran ina mpango wa kumuua balozi wetu, na wala hakusema kwamba amepewa ripoti hiyo na vyombo vya upelelezi. 

Swali linalojitokeza hapa ni kuwa, je Trump ana tatizo na taasisi za upelelezi za Marekani? Na je, vyanzo vilivyoashiriwa na jarida la POLITICO vipo kweli au ni vyanzo hewa na bandia?  
Suala jingine ni kwamba Donald Trump daima amekuwa akishambulia vyombo vya habari na kusema kuwa, vinasema uongo. Sasa imekuwaje anasadiki ripoti ya vyombo hivyo katika suala muhimu kama hili na kuchukua maamuzi kwa mujibu wa ripoti ya vyombo hivyo? Trump hakutosheka na vitisho hivyo, na kwa mara nyingine tena Alkhamisi iliyopita alihutubia wafuasi wake katika jimbo la Wisconsin akiashiria madai kwamba Iran ina nia ya kulipiza kisasi cha mauaji ya Kamanda Soleimani na kusema: "Tutatoa kipigo kikali mara elfu moja zaidi ya kile tulichokwishakitoa hadi sasa dhidi ya Iran." Trump alisema amekwishatoa maagizo ya maandishi kuhusu kadhia hiyo kwa maafisa na vyombo husika. Matamshi haya ya kijuba na yanayoakisi dhati ya kupenda vita na shari yanatolewa na mtu ambaye hivi karibuni wabunge wawili wa Ulaya walimpendekeza apewe tuzo ya amani ya Nobel!!

Kwa hahika Trump katika kipindi cha sasa cha utawala wake anavurumusha tuhuma za kila siku dhidi ya Iran kutokana na kushindwa mtawalia mkabala wa Jamhuri ya kiislamu hasa baada ya mpango wake wa kurefusha muda wa vikwazo vya silaha kukataliwa katika Baraza la Usalama na kupingwa hata na waitifaki wa Ulaya wa Marekani. Hii ni pamoja na kuwa Donald Trump mwenyewe anatambua vyema uwezo mkubwa wa kijeshi wa Iran hususan katika medani ya makombora kwa kadiri kwamba, Jamhuri ya Kiislamu inaweza kufanya mashambulizi makubwa na haribifu dhidi ya kambi na maslahi ya Marekani katika eneo la magharibi mwa Asia na kusababisha hasara kubwa za mali na nafsi. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Russia, Mikhael Shinkman anasema: Iwapo Marekani itafanya hujuma ya aina yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran itajikuta katika hali ambayo hakuna ajuaye jinsi ya kujinasua ndani yake.

Wakati huo huo Iran imetoa jibu mwafaka kwa tuhuma za Trump kupitia mwakilishi wake wa kudumu katika Umoja wa Mataifa mjini New York, Majid Takht-Ravanchi ambaye amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres na Rais wa Baraza la Usalama akilalamikia vitisho vya Rais wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.  

Majid Takht-Ravanchi, Mwakilishi wa Kudumu wa Iran UN

Msimamo wa wazi wa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Afrika Kusini wa kuhoji madai ya Marekani kwamba Iran ina mpango wa kumuua balozi wa nchi hiyo mjini Pretoria umedhihirisha kwamba tuhuma za Donald Trump hazina msingi wowote.   

Tags

Maoni