Sep 20, 2020 10:26 UTC
  • Madai ya Marekani kuhusu kurejeshwa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran; ndoto na kujidanganya kwake

Kugonga mwamba Marekani katika juhudi zake za kutaka muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran uongezwe katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuliifanya serikali ya Donald Trump sambamba na kuibuka na madai kuwa, ni mwanachama wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kwamba, Iran imekiuka makubaliano hayo, ilidai kurejea upya vikwazo vya kimataifa dhidi ya Tehran na ikatoa muhula wa mwezi mmoja katika uwanja huo

Wakati wa kumalizika muhula huo bandia, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani ilidai usiku wa kuamkia leo Septemba 20 kwamba, vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vikiwemo vya silaha vimerejea tena. Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani alitoa taarifa akisema eti Iran ndio tishio kubwa zaidi kwa eneo la Asia Magharibi na kudai kwamba, leo, Marekani inakaribisha suala la kurejeshwa vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Tehran ambavyo huko nyuma vilikuwa vimeondolewa.

Pompeo ameashiria kwamba, leo tarehe 20 Septemba, Marekani imemjulisha Mwenyekiti wa Baraza la Usalama kuhusiana na kutoheshimu Iran ahadi zake ilizojifunga nazo katika makubaliano ya JCPOA na kudai kwamba: Kwa msingi huo, vikwazo vimerejeshwa kwa mujibu wa utaratibu wa kurejesha tena vikwazo papo kwa papo, unaojulikana kitaalamu kama "Snapback Mechanism" ulioainishwa na azimio 2231.

Madai ya Marekani kuhusiana na kurejea vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran yanatolewa katika hali ambayo, nchi 13 wanachama wa kudumu na wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakiwemo wanachama wote wa kundi la 4+1 wanapinga vikali jambo hilo. Baraza la Usalama pia, siyo tu kwamba, halijatoa azimio kwa mujibu wa matakwa ya Marekani, bali limetekeleza mambo kinyume na matakwa ya serikali ya Trumpo kwani halijachukua hatua yoyote ile ya utangulizi ya kutekelezwa vikwazo hivyo kama vile kuunda kamati ya vikwazo na ya kitaalamu kwa ajili ya kutetekeleza hilo.

Mike Pompeo, Waziri wa MNashauri ya Kigeni wa Marekani

 

Wawakilishi wa Russia na Ufaransa katika Umoja wa Mataifa nao wamekosoa vikali hatua ya Marekani ya kuhuisha vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran na kusema kuwa, vikwazo hivyo kama ilivyokuwa huko nyuma vitabakia kuwa vimeondolewa.

Barbara Slavin, mkurugenzi wa mpango unaojuliakana kama Ubunifu wa Mustakabali wa Iran katika Chuo cha kifikra cha Baraza la Atalantic Marekani anasema kuwa, kwa kuzingatia kuwa, akthari ya mataifa ya dunia yanapinga ujengaji hoja wa kisheri wa Marekani na yamo mbioni kupuuza urejeshwaji wa vikwazo kwa kutumia utaratibu wa Snapback Mechanism, hakuna kitu kitakakachobadilika.

Kwa utaratibu huo, hatua ya Marekani ni madai yasiyo na mashiko na ni ya upande mmoja. Lengo kuu la Marekani kwa hatua zake zote hizi kimsingi ni kuzuia kuondolewa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran. Kuhusiana na jambo hilo, Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ametangaza bayana kwamba, sisi tumeanza kutekeleza haki zetu kwa mujibu wa utaratibu wa Snapback Mechanism kama ilivyo katika azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama ili kivitendo vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vilivyokuwa vimeondolewa vikwemo vya silaha tuvihuishe tena.

Marekani ikiwa na ndoto na hali ya kujidanganya kwamba, ndiyo polisi wa dunia inadhani kwamba, mataifa yote ya ulimwengu yanapaswa kufanya mambo yao kwa mujibu wa matakwa yake. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana baada ya kutangaza kutekeleza vikwazo hivi ikitumia mbinu yake ya siku zote yaani vitisho na vikwazo, sasa imeilenga dunia nzima kwa vitisho.

 

Katika taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani kumetolewa vitisho dhidi ya mataifa ya dunia endapo yatapinga utekelezwaji wa vikwazo hivi ambavyo ni madai ya bure bilashi na imebainishwa wazi kwamba, endapo nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa hazitatekeleza vikwazo hivi, basi Marekani iko tayari kutumia mamlaka ya ndani dhidi ya mataifa hayo ili iwe na uhakika kwamba, Iran hainufaiki kabisa na shughuli zilizopigwa marufuku na Umoja wa Mataifa.

Inaonekana kuwa, filihali Marekani haina budi badala ya kukabiliana na Iran ikabiliane na ulimwengu wote. Kwani kivitendo mbali na Marekani na mataifa madogo, hakuna dola lenye nguvu kimataifa iwe ni mashariki au magharibi mwa dunia na wanachama wengine wa Baraza la Usalama ambalo limeyatambua madai hayo ya Washington; na kimsingi madola hayo yamekuwa yakifanya mambo kinyume kabisa na msimamo huu wa Marekani.

Barbara Plett Usher, mwanahabari wa masuala ya kisiasa ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Takribani, wanachama wote wa Baraza la Usalama wanasema kuwa, hatua hiyo ni batili, kwani Marekani inatumia uratibu ambao upo katika makubaliano ya nyuklia na Iran, ambapo Washington si mwanchama tena wa makubaliano hayo. Hata hivyo Marekani imeonya kwamba, iko tayari kutekeleza hatua hii kwa kutumia vikwazo vya hatua ya pili kwa watu watakaopingana nayo.

Wakati huo huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza mara chungu nzima kwamba, hatua za Marekani dhidi ya Tehran si za kisheria.

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameashiria madai ya Marekani ya kurejesha tena vikwazo vilivyofutwa na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa na kusisitiza kwamba, muhula bandia iliotoa Marekani umeshapita na vikwazo hivyo havijarudi tena upya.

Majid Takht Ravanchi, Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa

 

Majid Takht Ravanchi amesema katika barua yake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kwamba, hatua ya Marekani ya kurejesha vikwazo vya baraza la Usalama si ya kisheria, batili na haitakuwa na taathira. Aidha amesema katika ujumbe alioandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, msimamo wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ungali ni ule ule kuwa Marekani si mwanachama tena wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, kwa hivyo madai ya kutekeleza utaratibu wa kurejesha tena vikwazo papo kwa papo, unaojulikana kitaalamu kama "Snapback Mechanism" ni batili na hayana uhusiano wowote na suala hilo. Kwenda kinyume na njia ya jamii ya kimataifa hakuna natija nyingine ghairi ya kutengwa.

Hii katika hali ambayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuwa, iko tayari kukabiliana na hatua yoyote tarajiwa ya Marekani katika kutekeleza madai yake haya yasiyo na msingi wowote.

Nukta nyingine ni hii kwamba, Donald Trump Rais mwenye chokochoko wa Marekani baada ya kushindwa mara kadhaa kuhusiana na masual ya ndani  na uungaji mkjono wake kupungua katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa Rais Novemba mwaka huu, anafanya kila awezalo kuongeza mashinikizo dhidi ya Iran na jamii ya kimataifa ili aonyesha kuwa amepata mafanikio makubwa katika uga wa kuongezea muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya  Iran kuptia utaratibu wa kurejesha tena vikwazo papo kwa papo, unaojulikana kitaalamu kama "Snapback Mechanism" au utaratibu wa kusuluhisha mzozano katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, unaojulikana kama 'Utaratibu wa Kifyatuo' kwa kimombo "Trigger Mechanism" na kwa njia hiyo ajiongezee hadhi na itibari mbele ya fikra za waliowengi hususan wapigakura nchini Marekani.

Kama alivyosema Hassan Kan’ani Moqaddam, mtaalamu wa masuala ya siasa za kigeni ni kuwa, wakati huu wa kukaribia uchaguzi wa Marekani, timu ya Trump inahaha kufa na kupona kutumia mashinikizo na hatua za upande mmoja hususan utaratibu wa kusuluhisha mzozano katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, unaojulikana kama 'Utaratibu wa Kifyatuo' kwa kimombo "Trigger Mechanism" ili kuongeza nafasi ya kiongozi huyo kushinda katika uchaguzi ujao wa Rais nchini Marekani.

Tags

Maoni