Sep 21, 2020 02:26 UTC
  • Khatibazadeh: Marekani inajua madai yake ya vikwazo dhidi ya Iran ni hewa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema tangazo la Marekani kwamba vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Tehran ambavyo vilikuwa vimeondolewa eti vimerejeshwa upya ni madai hewa, yasio na athari yoyote na yaliyo kinyume cha sheria.

Saeed Khatibzadeh alisema hayo jana Jumapili na kuongeza kuwa, Marekani inapaswa kuacha mienendo yake haribifu iwapo inataka kujiunga tena na jamii ya kimataifa baada ya kutengwa.

Amesema hatua zinazochukuliwa na utawala wa Washington hazijakuwa na matokeo mengine ghairi ya kusababisha ukosefu wa usalama na uthabiti, mbali na kuchochea vita katika maeneo mbalimbali duniani.

Khatibzadeh ametoa matamshi hayo baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo kutangaza kuwa eti vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vimerejea tena kuanzia jana Jumapili.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza bayana kuwa, matamshi ya Pompeo ya kurejeshwa vikwazo vya UN dhidi ya Iran ni ya uongo na hayana msingi wowote; na kwamba washirika watatu wa Marekani katika Umoja wa Ulaya wametoa taarifa ya kupuuzilia mbali bwawaja hizo za  Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo

Jana Jumapili, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi tatu za Ulaya za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza walitoa tamko la pamoja na kusema kuwa, Troika ya Ulaya itaendelea kuheshimu azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopasisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA na haitojali madai ya Marekani kuwa vikwazo hivyo vimerejea vyenyewe. 

Kadhalika Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema EU itaendelea kuheshimu mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kwamba Marekani haina haki ya kuchukua hatua ya upande mmoja ya kurejesha vikwazo hivyo dhidi ya Iran kwa kuwa si mshiriki tena wa makubaliano hayo ya kimataifa.

Tags

Maoni