Sep 21, 2020 03:17 UTC
  • Rouhani: Kutengwa zaidi, matunda ya mashinikizo ya juu zaidi ya Marekani dhidi ya Iran

Rais Hassan Rouhani ameashiria kuhusu kugonga mwamba njama za Marekani dhidi ya taifa la Iran na kueleza bayana kuwa: Hatua za Washington mkabala wa Iran hazijakuwa na matokeo mengine isipokuwa kuifanya nchi hiyo itengwe zaidi katika uga wa kimataifa.

Rais Rouhani alisema hayo jana Jumapili katika kikao cha Baraza la Mawaziri na kuongeza kuwa: Wamarekani wameshindwa kuunda muungano dhidi yetu. Mashinikizo ya juu zaidi ya Marekani dhidi ya Iran katika nyuga za kisiasa na kisheria yamepelekea kutengwa zaidi Washington.

Amebainisha kuwa, iwapo Marekani inataka kujiingiza katika mchezo wa kuburuzana, ijiandae kupokea jibu mwafaka kutoka kwa Iran ya Kiislamu.

Dakta Rouhani ameeleza bayana kuwa, tangu Marekani ijiondoe kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA, maafisa wa Washington wamekuwa wakienda mbio kujaribu kuzivutia upande wao nchi za Umoja wa Ulaya, na wakadhani kwamba, kwa kuichokoza Jamhuri ya Kiislamu, wataandaa mazingira ya kurejeshwa vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.

Amesema jitihada za Marekani ndani ya miezi kadhaa iliyopita, za kutaka kulitumia Baraza la Usalama kutoa pigo kwa Iran zimefeli na kuifanya nchi hiyo ya kibeberu itengwe zaidi hata na marafiki na waitifaki wake mashuhuri.

Marekani imeshindwa kuwashawishi hata waitifaki wake katika Baraza la Usalama la UN dhidi ya Iran

Rais Hassan Rouhani amekumbusha kuwa, kamwe taifa la Iran halitaipigia magoti Marekani kutokana na tabia yake ya kupenda makuu na kutumia mashinikizo na vikwazo. Amebainisha kuwa,"siku zote tumekuwa tukisema kuwa kuna njia moja tu ya kuamiliana na taifa la Iran, na njia hiyo ni kuheshimu haki za taifa la Iran na kulizungumzia kwa lugha ya heshima."

Rais wa Iran amesema taifa hili halijawahi na katu halitowahi kusalimu amri mbele ya mashinikizo na ubeberu wa Marekani katika hali yoyote ile. Ameongeza kuwa, kupiga mweleka Marekani mkabala wa Iran kumetokana na kusimama kidete Wairani.

Tags

Maoni