Sep 21, 2020 06:14 UTC
  • Kulipiza kisasi cha kuuliwa shahidi Luteni Jenerali Qassim Suleimani; uhakika uliokwisha amuliwa na usio na mzaha

Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye hadi sasa amesha jaribu kutumia mbinu tofauti ili kuitisha na kuitia hofu Iran, katika siku za karibuni ameibuka tena na kutoa maneno mengine ya vitisho dhidi ya taifa hili.

Jarida la POLITICO linalochapishwa huko Marekani, wiki iliyopita, na bila kuonyesha ushahidi wowote, lakini kwa ajili tu ya kumpatia fursa Trump ya kutamba na kuonyesha ubabe kabla ya kufanyika uchaguzi wa urais wa nchi hiyo wa tarehe 3 Novemba, lilidai kwamba Iran imedhamiria kumuua balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini ili kulipiza kisasi cha mauaji ya kigaidi ya kamanda Qassim Suleimani.

Luteni Jenerali, Shahidi Qassim Suleimani

Kwa kutegemea madai hayo ya kipuuzi na yasiyo na maana, Trump alisema katika hotuba aliyotoa mbele ya hadhara ya wafuasi wake katika jimbo la Wisconsin: "Sisi tutawapa kipigo kikali zaidi mara elfu kuliko tulichowapiga hadi sasa."

Brigedia Jenerali Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) alitoa jibu kwa bwabwaja hizo za rais wa Marekani dhidi ya Iran kwa kusisitiza kwamba: "Ulipizaji kisasi cha kuuliwa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani ni uhakika ambao umesha amuliwa na si wa mzaha."

Kamanda Mkuu wa IRGC, Brigedia Jenerali Hussein Salami 

Mauaji ya kigaidi ya Luteni Jenerali Qassim Suleimani yaliyofanywa mwezi Januari mwaka huu, katika hali ambayo jemadari huyo alikuwa ameelekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo, yailikuwa tusi na dharau kubwa kwa mamlaka ya kujitawala ya Iraq yenyewe na pia ilikuwa ni jinai kubwa sana liliyotendewa taifa la Iran. Baada ya kupita siku tano tangu kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassim Suleimani na wanamapambano wenzake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitoa jibu la kwanza kwa kitendo hicho cha kigaidi kwa kukishambulia kwa makombora makali kituo cha anga cha Ainul-Asad, ambayo ndiyo kambi kubwa zaidi na yenye umuhimu mkubwa zaidi kwa Marekani nchini Iraq.

Kuhusiana na mauaji hayo ya kigaidi yaliyofanywa na Marekani, Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran limeagiza kuchukuliwa "uamuzi unaofaa"; na ndiyo kusema kwamba Marekani ikae ikijua, wakati wowote na mahali popote patakapoonekana kuwa ni mwafaka, itakabiliwa na hatua ya ulipizaji kisasi ya Iran.

Kituo cha anga cha Ainul Asad baada ya kushambuliwa  na Iran kwa makombora 

Nukta muhimu katika kutathmini jibu kali la Iran kwa kitisho cha aina yoyote na cha kiwango chochote kiwacho ni utayarifu wake wa kujihami na kumzuia adui asithubutu kushambulia pamoja na nguvu na uwezo wake wa kushambulia kwa ajili ya kuzima vitisho dhidi yake.

Hotuba ya Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambayo ni ya kujibu vitisho alivyotoa Trump ina umuhimu mwingine pia kutokana na nukta kuu na za kistratejia zilizomo ndani yake kuhusiana na utambuzi kamili wa hali na mazingira magumu yanayoikabili Marekani katika eneo. Brigedia Jenerali Salami  ameeleza katika hotuba yake kwamba, hii leo mgao wa Marekani dunia unaendelea kudogeka kwa sababu madola mapya yenye nguvu yanaendelea kujitokeza; na Uislamu umejitokeza kama nguvu moja kubwa na yenye nafasi katika sura ya Ustaarabu.

Anthony Kurtzmann, mchambuzi katika kituo cha mitaala ya kistratejia na kimataifa cha Washington anaashiria uwezo wa kijeshi wa Iran na kusema: "Endapo zitaanzishwa chokochoko zozote za kijeshi dhidi ya Iran, Tehran itasababisha zilzala ya kimawimbi katika eneo, kwa sababu ina mikakati mingi ya kijeshi ya kulenga maslahi ya Marekani katika eneo." 

Makombora ya Iran ya Naseer ya kutoka ardhini kuelekea baharini yanayolenga umbali wa kilomita 700

Makao makuu ya vikosi vya ulinzi vya Iran, nayo pia yalitoa taarifa maalumu siku ya Jumamosi kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka wa 40 wa kumbukumbu za Kujihami Kutakatifu kwa kutilia mkazo kuhusu nguvu na uwezo huo. Kwa hivyo hotuba iliyotolewa na Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu inakumbusha tena vielelezo vya uwezo na nguvu katika Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wakati huohuo ni jibu madhubuti kwa bwabwaja za kujifanya mbabe za Trump ambaye anadhani anaweza kulitia hofu taifa la Iran kwa kutoa kauli za vitisho.../

Maoni