Sep 22, 2020 02:36 UTC
  • Muhammad Javad Zarif
    Muhammad Javad Zarif

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran sambamba na maadhimisho ya kumbukumbu ya kuanza vita vya kulazimishwa vya utawala wa Baath wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa: Wananchi wa Iran wanasimama kwa fakhari miaka 40 baada ya mashambulizi ya Saddam yaliyoungwa mkono na kusaidiwa na nchi mbalimbali.

Muhammad Javad Zarif jana Jumatatu aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwa mnasaba wa kuwakumbuka mashahidi wa miaka minane ya vita vya kujitetea kutakatifu kwamba: Wale wanaoanzisha vita, hawataweza kuvihitimisha, na vita havina mshindi.

Jumatatu ya jana tarehe 21 Septemba mwaka 2020 imesadifiana na kumbukumbu ya kuanza vita vya kutwishwa vilivyoanzishwa na utawala wa Saddam dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.  

Jeshi vamizi la utawala wa Saddam Hussein dikteta aliyeng'olewa madarakani huko Iraq, tarehe 31 mwezi Shahrivar mwaka 1359 Hijria Shamsia sawa na mwezi Septemba mwaka 1980, lilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Iran kwa kutumia aina mbalimbali za silaha likidhani kwamba katika muda wa wiki moja tu lingeweza kuudhibiti mji wa Tehran.  

Dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein 

Katika muda wote wa miaka minane ya vita kati yake na Iran ya Kiislamu jeshi la utawala wa Saddam lilisaidiwa na kuungwa mkono kwa pande zote na madola ya kibeberu na kupatiwa misaada chungu nzima na nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi. 

Wananchi wa Iran katika kipindi cha miaka minane ya kujitetea kutakatifu, walidhihirisha kuwa, licha ya vizuizi, mashinikizo na uhaba wa fedha na matatizo mengine mengi, wanaweza kusimama imara dhidi ya ubeberu na dhulma ya madola kandamizi duniani kwa azma thabiti na kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu. 

Maoni