Sep 23, 2020 09:53 UTC
  • Kubainisha utambulisho halisi wa Marekani; mhimili wa hotuba ya Rais Rouhani katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Mwaka huu mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unafanyika katika mazingira maalumu kutokana na kuenea ulimwenguni kote virusi vya corona.

Mkutano huu wa 75 ambao mwaka huu unafanyika kwa njia ya video, ni fursa nzuri ya kubainisha daghadagha na wasiwasi unaoukabili ulimwengu hivi sasa.

Akihutubia kwa njia ya video kupitia mawasiliano ya intaneti katika huo, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya kiislamu ya Iran amebainisha mitazamo na misiamo ya Iran kuhusiana na masuala mbalimbali yanayoukabili ulimwengu hivi sasa sambamba na kuweka wazi utambulisho halisi wa Marekani pamoja na matokeo ya uchukuaji maamuzi ya upande mmoja.

Hotuba ya Rais Hassan Rouhali ilitilia mkazo masuala mawili muhimu:

Jambo la kwanza; alitilia mkazo nukta hii kwamba, taifa la Iran katu halitasalimu amri mbele ya ubabe na utumiaji mabavu wa Marekani na hili limethibiti kivitendo. Taifa la Iran lina historia ya maefu ya karne na haliwezi kuruhusu dola la kimabavu la Marekani liamiliane na taifa hili kadiri linavyotaka. Rais Hassan Rouhani sambamba na kubainisha kwamba, "Marekani haiwezi kutulazimisha kufanya mazungumzo wala kuanzisha vita dhidi yetu" amesisitiza kwamba, sasa ni wakati wa walimwengu kusema "hapana" kwa ubabe na utumiaji mabavu.

 

Jambo la pili lililobainishwa na Rais Rouhani katika hotuba yake katika mkutano wa mwaka huu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni undumakuwili na mgongano wa Marekani ambao umeligeuza taifa hilo na kuwa hatari na tishio kwa usalama wa dunia. Sehemu ya undumakuwili huu ni unahusiana na haki za binadamu. Kuhusiana na suala la haki za binadamu, kuna undumakuwili mkubwa katika mtazamo wa Magharibi. Kile ambacho kinashuhudiwa leo katika jamii ya Marekani, ni mfano wa wazi katika uwanja huu.

Wananchi wa Marekani wamechoshwa na ubaguzi wa rangi, ufisadi, dhulma, ukosefu wa uadilifu na uzembe na kutokuwa na uwezo viongozi na hii leo walimwengu wote wanasikia sauti yao ya malalamiko.

Kuhusiana na teknolojia ya nishati ya atomiki pia, ambayo ni matunda ya miaka kadhaa ya juhudi na idili ya wasomi na wataalamu wa Kiirani kwa ajili ya kunufaika na teknolojia hiyo kwa malengo ya amani, tunashuhudia vikwazo na upinzani wa Marekani ulio nje ya ada na mazoea. Hatua hizo za Marekani siyo tu kwamba, hazina hoja za kimantiki bali hazina mashiko ya kisheria pia. Hatua za Marekani ni za kueneza ukiukaji wa sheria ambapo natija yake ni kuukalia kichwani Umoja wa Mataifa na kupuuza maazimio ya Baraza la Usalama.

Noam Chomsky, mwanafikra na mwananadharia mtajika wa Kimarekani

 

Marekani ikiwa taifa pekee ulimwenguni lililotumia silaha za atomiki dhidi ya raia, limekuwa kikwazo na kizingiti kikuu cha ulimwengu kusafishwa na kutokuwa na silaha za atomiki. Ikulu ya Marekani White House imewasaidia washirika wake kama utawala dhalimu wa Israel ili umiliki na kupanua viwanda vya nyuklia na kufumbia macho kikamilifu shughuli zisizo za kawaida za atomiki za Israel na utawala wa Saudi Arabia.

Noam Chomsky, mwanafikra na mwananadharia mtajika wa Kimarekani, sanjari na kuashiria sehemu ya undumakuwili huu katika sera na siasa za Washington anasema: Ukosefu wa amani una maana ya ajabu katika mazungumzo ya kisiasa. Wakati Iran inapopambana na kundi la kigaidi la Daesh Asia Magharibi, hatua hii inatajwa kuwa ni kuvuruga amani na usalama, lakini wakati Marekani inapoishambulia kijeshi Iraq na kuwauwa mamia ya maelfu ya raia wa nchi hiyo, kuwafanya mamilioni miongoni mwao kuwa wakimbizi, inapoangamiza nchi, inapozusha vurugu za kikabila na kuigawa Iraq na kupelekea eneo lote la Asia Magharibi kukumbwa na mizozo, inapoeneza ugaidi katika maeneo mbalimbali ya dunia, hayo yote huonekana kuwa eti ni sehemu ya ujumbe wa Marekani wa kuleta amani na uthabiti duniani.

Image Caption

 

Katika mazingira kama haya, kukabiliana na siasa za upande mmoja za Marekani, bila shaka ni hitajio la kilimwengu na jamii ya kimataifa inapaswa kutafuta njia ya kukabiliana na siasa hizi za kibabe, ili izuie jambo hilo kutogeuzwa na kuwa ada na mazoea katika mahusiano ya kimataifa. Hotuba ya Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa hakika imebainisha taathira za uchukuaji maamuzi ya upande mmoja wa Marekani kwa mustakabali wa dunia ambazo zimejificha katika nara na kaulimbiu zenye hadaa kama vile kulinda usalama, demokrasia na haki za binadamu ulimwenguni.

Maoni