Sep 24, 2020 02:42 UTC
  • Kamanda Fadavi: Marekani haitoweza kuunda muungano dhidi ya Iran

Kaimu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kuwa, njama za Marekani za kuunda muungano ulio dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zitashindwa tu.

Kamanda Ali Fadavi alisema hayo jana Jumatano wakati alipohojiwa na televisheni ya al Mayadeen na kusema kuhusu njama za Marekani za kuunda muungano ulio dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba, hii si mara ya kwanza kwa Marekani kufanya njama hizo, huko nyuma pia ilifanya njama mbalimbali kama hizo lakini haijawahi kufanikiwa hata mara moja.

Kaimu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH vile vile amesema, ni bora kwa wanajeshi wa Marekani kujileta wenyewe kwenye eneo hili la Ghuba ya Uajemi kwani watakuwa ni shabaha rahisi kwa wanajeshi shujaa wa Iran ya Kiislamu. Amesema kama Wamarekani watafanya kosa jingine lolote la kipumbavu, watajibiwa kwa namna wasioyoitarajia kabisa.

Donald Trump, rais wa Marekani

 

Kamanda Fadavi aidha amesema kwa kusisitiza kwamba, Marekani itashindwa pia kufikia malengo ya njama zake za kutaka kuiwekea vikwazo vya silaha Iran kama ambavyo imeshindwa pia katika njama zake nyingine zote. 

Itakumbukwa kuwa, Jumamosi wiki hii, Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH alisema kwamba jeshi hilo litachukua hatua kali ya kulipiza kisasi cha mauaji ya kigaidi yaliyofanywa kwa amri ya rais wa Marekani, Donald Trump dhidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kumhutubu rais huyo wa Marekani akimwambia: Trump! usiwe na shaka hata kidogo kuhusu kisasi chetu, hilo ni jambo lisilo na shaka na ni ukweli mtupu."

Tags

Maoni