Sep 25, 2020 06:36 UTC
  • Ukurasa mpya wa ushirikiano wa kibiashara kati ya Iran na Afghanistan

Ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Afghanistan upo katika mkondo wa kupiga hatua na katika uwanja huo, na kwa mara ya kwanza kumefanyika maonyesho ya kitaalamu ya Iran kwa muda wa siku tatu katika mji mkuu wa Afghanistan Kabul.

Maonyesho ya kwanza ya kitaalamu ya Iran katika sekta ya huduma za kiufundi na kiuhandisi za nishati, umeme, posta na simu na huduma za miji yamefanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 22 Septemba na kumalizika jana Alkhamisi tarehe 24.

Mashirika 21 ya Kiirani katika sekta ya huduma za miji na mashirika 54 ya Kiirani katika sekta ya huduma za kiuhandisi na kiufundi yameshiriki katika maonyesho hayo ya Kabul. Sambamba na maonyesho hayo, ujumbe mkubwa wa Iran uliojumuisha wafanyabiashara 150 na wawakilishi kadhaa wa Bunge la Iran walifanya safari katika mji mkuu huo wa Afghanistan na ukiwa uko ulikutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara, maafisa wa serikali na wawakilishi wa Bunge la nchi hiyo. Pande mbili hizo zilibadilishana mawazo kuhusiana na masuala mbalimbali hususan masuala ya biashara na uwekezaji.

Hafla ya ufunguzi wa maonyesho ya kwanza ya kitaalamu ya Iran mjini Kabul

 

Safari ya ujumbe mkubwa kama huu wa Iran mjini Kabul na kufanyika maonyesho ya kwanza ya kitaalamu katika sekta ya ufundi na uhandishi wa Iran nchini Afghanistan ni ishara ya wazi ya kufunguliwa ukurasa mpya katika ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi mbili hizi jirani.

Kuweko mafungamano ya kiutamaduni, kijiografia, kihistoria na kistaarabu baina ya Iran na Afghanistan, ni mambo yanayoziweka nchi mbili hizi katika mkondo mpya wa ushirikiano wa kibiashara ambapo kufanyika maonyesho ya kwanza ya kitaalamu katika sekta ya ufundi katika mji wa Kabul ni ubunifu athirifu kwa ajili ya kupanua kiwango cha biashara baina ya Iran na Afghanistan.

Filihali Afghanistan na Iran zina ushirikiano mzuri katika sekta ya mabadilishano ya kibiashara, hata hivyo kwa uamuzi wa viongozi wa nchi mbili, kiwango hiki cha ushirikiano kinaingia katika hatua na marhala mpya ambayo bila shaka itasaidia ustawi wa kielimu nchini Afghanistan. Kupatiwa Afghanistan tajiriba na teknolojia ya Iran ya huduma za kiufundi na kiuhandisi katika nyanja mbalimbali hususan katika uga wa nishati, ni mambo ambayo yatasaidia sana katika kupanua na kuimarisha miundomsingi ya Afghanistan.

Bendera za Iran (kushoto) na Afghanistan

 

Kuhusiana na suala hilo, Bahador Aminiyan balozi wa Iran mjini Kabul akibainisha umuhimu wa kufanyika maonyesho ya kitaalamu katika masuala ya kiufundi na kiuhandishi katika mji mkuu wa nchi hiyo amesema kuwa, katika kipindi cha miaka mingi ya huko nyuma, Iran imekuwa na mahusiano mazuri ya kibiashara na Afghanistan na katika marhala hii mpya, Tehran inafuatilia kuimarisha uhusiano huo kupitia mafungamano ya kiteknolojia na huduma za kiuhandisi.

Katika miaka ya hivi karibuni, Iran ikitegemea utaalamu wa wasomi na wataalamu wake wa hapa ndani imeweza kupiga hatua nzuri katika uga wa teknolojia na kuweko hapa nchini mamia ya shughuli za mashirika na taasisi za elimumsingi, imeandaa uwanja mzuri kwa ajili ya nchi jirani kuweza kunufaika na tajiriba hii ya elimu na teknolojia ya kisasa.

Moja ya safari za Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan mjini Tehran

 

Kustafidi mataifa jirani na elimu na utaalamu huu, ni fursa mpya kwa ajili ya kustawisha elimu na kutatua matatizo na katika uga huu, kizazi cha vijana cha Afghnaistan kinaweza kunufaika na tajiriba ya wataalamu wa Iran katika nyuga za teknolojia na hivyo kuweza kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayoikabili nchi hiyo jirani.

Kuingia biashara ya Iran na Afghanistan katika hatua mpya ya kiufundi na kiuhandisi ni kwa maslahi ya ustawi na ujenzi wa nchi hiyo jirani; na katika anga ya amani na usalama, Afghanistan inaweza kuongeza siku baada ya siku kiwango cha ushirikiano baina ya pande mbili hizi.

Tags

Maoni