Sep 25, 2020 11:15 UTC
  • Zaidi ya wagonjwa 3,000 wapya wa corona wagunduliwa nchini Iran

Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran ametangaza kuwa, zaidi ya wagonjwa wapya elfu tatu (3,000) wa COVID-19 wamegunduliwa humu nchini katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita.

Daktari Sima Sadat Lari, amesema hayo leo wakati akitoa takwimu mpya za watu waliokumbwa na kirusi cha corona hapa Iran na kuongeza kuwa: Kwa mujibu wa matokeo ya vipimo rasmi, katika muda wa masaa 24 yaliyopita wagonjwa wapya 3,563 waliokumbwa na ugonjwa wa COVID-19 wamegunduliwa humu nchini, ambapo 1,708 miongoni mwao wamelazwa hospitalini na waliosalia wamepatiwa huduma za tiba na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Bi Lari amefafanua kuwa, idadi ya watu waliogunduliwa kupatwa na ugonjwa wa COVID-19 nchini Iran hadi hivi sasa imefikia 439,882  na kutokana na wagonjwa 207 kuaga dunia katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, jumla ya watu waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huo hadi sasa hapa nchini imefikia 25,222.

 

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran hadi kufikia leo mchana, wagonjwa 369,842 wamepata afueni na kuruhusiwa kutoka hospitalini na kurejea majumbani.

Wakati huo huo, hadi kufikia leo mchana, idadi ya watu waliokumbwa na kirusi cha corona duniani kote imepindukia milioni 32. Miongoni mwa hao, watu zaidi ya 998,000 wameshaaga dunia na wengine milioni 24 wamepata nafuu na kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Marekani imeendelea kuwa nchi iliyoathiriwa zaidi na kirusi cha corona duniani, ikifuatiwa na India, Brazil, Russia, Colombia Peru na Mexico.

Tags

Maoni