Sep 26, 2020 10:20 UTC
  • Taarifa ya Umoja wa Ulaya dhidi ya Iran; mwendelezo wa misimamo ya kindumakuwili kuhusu haki za binadamu

Nchi za Magharibi zimekariri tena madai yao ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Iran wakati idadi kubwa ya nchi hizo, kama Ufaransa na Uingereza, zimewekwa kwenye orodha ya wakiukaji wa haki hizo za binadamu.

Ijumaa ya jana Umoja wa Ulaya ulitoa taarifa ya kichochezi katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kuituhumu Iran huwa inakiuka haki za binadamu. Harakati hii inaweza kuwa na melengo mawili makuu. 

Kwanza ni kutumia haki za binadamu kama wenzo wa mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Lengo la pili ni kutaka kusisitiza mshikamano na ushirikiano wa kisiasa wa Umoja wa Ulaya na Marekani. Ushirikiano na mshikamano huo unaonekana vyema zaidi katika masuala kama ya haki za binadamu, uwezo wa makombora ya Iran na nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu katika kanda ya magharibi mwa Asia.

 Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Iran Saeed Khatibzadeh amejibu tuhumu hizo akisema kuwa utumiaji mbaya wa aina yoyote wa masuala ya haki za binadamu na kuingilia masuala ya ndani ya Iran haukubaliki. Khatibzadeh amesisitiza kuwa: "Si jambo jipya kuona baadhi ya nchi za Ulaya zikanyamazia kimya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na nchi hizo na washirika wao. Nchi hizi zinashindana kuuza silaha za mabilioni ya dola kwa Saudi Aabia na madikteta wengine wa kanda hii, silaha ambazo zinatumiwa kuua raia wasio na hatia wa Yemen."

Saeed Khatibzadeh

Nchi hizo za Magharibi zinatoa tuhuma za kukiuka haki za binadamu dhidi ya nchi nyngine huku zikendelea kutambua uhalifu kama wa kukandamiza waandamanaji, mauaji ya watu weusi, kuvunjia heshima matukufu ya kidini, kuwadhalilisha Waislamu na kuwakandamiza wahajiri ndani ya mipaka ya nchi za Ulaya kuwa ni utekelezaji wa sheria na uhuru wa kusema na kujieleza! Ukweli ni kwamba utendaji wa Umoja wa Ulaya katika suala la haki za binadamu, sawa kabisa na ule wa Marekani, hauwezi kutetewa na kuhalalishwa kwa njia yoyote ile. Hii ni kwa sababu taswira ya haki za binadamu barani Ulaya hususan kuhusu ukandamizaji wa maandamano ya wananchi, imejaa  picha za kutisha na kusikitisha sana na mienendo isiyo ya kibinadamu.

Vigezo vya kindumakuwili vya nchi za Ulaya kuhusu haki za binadamu pia vimepingwa vikali na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International. Ripoti iliyochapishwa mwaka jana na shirika hilo iliukosoa Umoja wa Ulaya na kusema: Umoja huo unanyamazia kimya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanyika katika baadhi ya nchi.

Sehemu moja ya ripoti ya Amnesty International ilisema: "Umoja wa Ulaya umenyamaza kimya na haujachukua hatua yoyote ya kupinga ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanyika nchini Saudi Arabia licha ya kwamba wapinzani nchini humo wanabinywa na kukandamiza vikali. EU imefadhilisha suala la kulinda uhusiano wa nchi wanachama na utawala wa kifalme wa Saudia kuliko kutetea haki za binadamu zinazokanyagwa nchini humo."

Silha zinazouzwa kwa Saudia zimeua maelfu ya watoto wa Yemen

Mienendo hiyo ya kindumakuwili inaonyesha kuwa, watayarishaji wa taarifa ya nchi za Magharibi katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa wanajaribu kuficha sura zao halisi  kupitia njia ya kuituhumu Iran kuwa inakiuka haki za binadamu. Taarifa hiyo ya Umoja wa Ulaya kwa hakika ni mwendelezo wa harakati za kisiasa zinazofanyika kwa shabaha ya kuzihadaa na kuzipotosha fikra za walimwengu. Katika upotoshaji wa waziwazi, taarifa ya Umoja wa Ulaya katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, imeutaja utekelezaji wa sheria za adhabu katika mahakama stahiki katika nchi nyingine kuwa ni ukiukaji wa haki za binadamu. Hata hivyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, bila ya kujali upotoshaji na propaganda hizo chafu, itaendelea kulinda na kuboresha haki za raia wake kwa kutilia maanani sheria aali za dini ya Uislamu na Katiba ya nchi. Ni kwa kuzingatia suala hilo ndipo Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran akasema kuwa: Suala la kustawisha na kuboresha haki za binadamu kitaifa, kikanda na kimataifa katika fremu ya mafundisho ya dini, Katiba na sheria za nchi, ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele zaidi katika Jamhuri ya Kiislamu. 

Tags

Maoni