Sep 27, 2020 04:08 UTC
  • Kurejea kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA, hatua ya kwanza inayopasa kuchukuliwa na Marekani

Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akiyataja mapatano ya nyuklia ya JCPOA kuwa ndiyo mapatano mabaya zaidi kwa nchi yake na hatimaye mwezi Mei mwaka 2018 aliiondoa nchi hiyo kwenye mapatano hayo na kuiwekea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikwazo vikali. Hivi sasa Joe Biden mgombea wa kiti cha urais wa chama cha Democratic huko Marekani amesema iwapo atashinda uchaguzi huo wa mwezi Novemba mwaka huu atairejesha Marekani katika mapatano hayo ya JCPOA.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amezungumzia suala hilo katika mahojiano yake na shirika la habari la Sputnik akisema: kurejea Marekani katika mapatano ya JCPOA ndiyo hatua ya kwanza inayopasa kuchukuliwa na Washington, na Marekani inalazimika kuilipa Iran hasara zilizosababishwa na hatua yake ya kujitoa kwenye JCPOA. Vilevile Washington inapaswa ifidie madhara yote yaliyosababishwa na hatua ilizochukua kudhoofisha mapatano hayo ya nyuklia. 

Matamshi hayo ya Dakta Zarif yameashiria ahadi iliyotolewa na Joe Biden ya kuirejesha Marekani kwenye mapatano ya JCPOA iwapo ataibuka mshindi katika uchaguzi wa Novemba mwaka huu. Mwezi uliopita Biden alizitaja sera na siasa za Trump mkabala na Iran kuwa zilizofeli na kushindwa na akasema kwamba iwapo atashinda uchaguzi wa rais atakhitari njia ya kuaminika ya kuamiliana kidiplomasia katika uhusiano na Iran. Katika maandishi yake ya karibuni Biden alisema kwamba Trump amefanya makosa kujiondoa kwenye mapatano ya JCPOA na alichukua hatua inayopingana na maslahi ya kitaifa na kuifanya Marekani itengwe zaidi. 

Mapatano ya nyuklia ya JCPOA yaliyopasishwa na Baraza la Usalala la UN 

Naibu Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ambaye kwa sasa ni Mshauri wa Biden katika siasa za nje amesema: iwapo Iran itaheshimu kikamilifu mapatano ya nyuklia ya JCPOA serikali ya Biden, iwapo atashinda uchaguzi wa rais, itarejea pia katika mapatano hayo. Tunaweza kwa kushirikiana na washirika wetu kufanya juhudi kubwa zaidi kuyaimarisha mapatano hayo na kuyafanya ya muda mrefu zaidi.  

Antony Blinken, Naibu Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani

Hatua ya Biden ya kukiri kwamba Trump ameshindwa katika siasa zake za kukabiliana na Iran zinaonyesha kuwa hata wanasiasa wa ngazi za juu zaidi wa Marekani wametambua kwamba licha ya madai ya mara kwa mara ya maafisa wa serikali ya Trump khususan Mike Pompeo kwamba kampeni ya mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi imeifanya hali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ngumu zaidi, lakini kivitendo Iran imeweza kusimama imara mbele ya mashinikizo hayo ya kiwango cha juu kwa kutumia stratejia ya muqawama wa kiwango juu na imefanikiwa kuzima njama za Marekani za kutaka kurefusha vikwazo vya kimataifa dhidi yake. Zaidi ni kwamba kwa sasa serikali ya Trump imekumbwa na hali ya kutengwa kwa kiwango cha juu zaidi katika upeo wa kimataifa.

Alex Watankhah, Mkurugenzi wa Programu ya Iran katika Taasisi ya Magharibi mwa Asia mjini Washington anasema: "Marekani imebaki na kuachwa pekee yake katika makabiliano yake na Iran.  
Misimamo ya Biden inaonyesha kwamba mwanasiasa huyo pia ana mitazamo inayofanana na Trump katika suala la udharura wa kuondolewa kile kinachotajwa kuwa ni wasiwasi kuhusu mipango ya nyuklia yenye malengo ya amani ya Iran na masuala mengineyo, lakini Biden anatafuta njia nyingine tofauti na ya Trump ili kutatua masuala haya. Nukta muhimu inayopasa kusisitizwa ni kwamba, katika kipindi cha miaka 40 iliyopita marais wote wa Marekani, wawe wa Democrat au Warepublican, wamekuwa na mienendo ya kihasama na ya kuiwekea mashinikizo Iran khususan katika masuala ya vikwazo. Serikali ya Barack Obama pia licha ya kushiriki katika kundi la 5+1 katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA iliweka au kudumisha vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na haikutekeleza majukumu yake katika mapatano hayo.

Joe Biden, mgombea wa urais wa chama cha Democrat 

Hivi sasa pia Biden ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa Obama anadai kwamba atairejesha nchi hiyo katika mapatano ya JCPOA iwapo ataingia ikulu ya White House. Pamoja na hayo anasisitiza kwamba katika utawala wake Washington ikishirikiana na washirika wake itafanya jitihada za kuweka vizingiti zaidi katika mapatano ya JCPOA na kuyarefusha mapatano hayo. Vile vile atashughulikia masuala mengine ya Iran yanayoitia wasiwasi Washington. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa Biden kama alivyokuwa Barack Obama anataka kujumuisha masuala mengine katika mapatano ya JCPOA kama suala la uwezo wa makombora ya Iran, siasa za kikanda za Jamhuri ya Kiislamu na masuala ya haki za binadamu. Mkabala wake, Iran imekuwa ikisisitiza kwamba itaendelea kuheshimu mapatano ya JCPOA tu na abadan haitasalimu amri kwa matakwa ya Washington katika masuala yanayohusiana na uwezo wa makombora yake, siasa zake katika kanda ya Magharibi mwa Asia, haki za binadamu na mfano wa hayo.

Tags

Maoni