Sep 27, 2020 08:03 UTC

Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema shambulizi la jeshi la Marekani lililoua shahidi mashujaa wa kupambana na ugaidi katika eneo la Asia Magharibi mapema mwaka huu ni tusi kwa mamlaka ya kujitawala Iraq.

Muhammad Baqir Qalibaf amesema hayo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Fuad Hussein, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iraq na kuongeza kuwa, mamlaka ya kujitawala Iraq ulikanyagwa kutokana na shambulizi la kigaidi la Marekani lililoua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Walinzi wa Mapiduzi ya Kiislamu (SEPAH) na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu wa Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq al Hashd al Shaabi. 

Qalibaf amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikiunga mkono mamlaka ya kujitawala, uhuru na usalama wa Iraq na kuitazama nchi hiyo ya Kiislamu kama jirani muhimu.

Luteni Jenerali Qassem Soleimani,  Abu Mahdi al Muhandis pamoja na wenzao wengine wanane waliuliwa shahidi usiku wa kuamika Ijumaa tarehe 3 Januari katika shambulio la anga lililofanywa na utawala wa kigaidi wa Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad, mji mkuu wa Iraq.

Spika wa Bunge la Iran ameongeza kuwa, suluhu ya matatizo na changamoto za kiusalama zinaoikabili Iraq ni kuondoka wanajeshi vamizi wa Marekani katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Mashahidi Solaimeni na Muhandes

Kadhalika Muhammad Baqir Qalibaf amebainisha kuwa, ulimwengu wa Kiislamu haupaswi kunyamazia kimya kitendo cha Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain cha kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na kuongeza kuwa, kadhia ya Palestina ndilo suala muhimu zaidi hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu.

Kwa upande wake, Fuad Hussein Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iraq amesisitizia haja ya kuboreshwa zaidi uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Baghdad, kutokana na nchi mbili hizi jirani kuwa na maslahi ya pamoja katika nyuga za kisiasa na kiuchumi.

 

Tags

Maoni