Sep 27, 2020 13:06 UTC
  • Iran yazindua kombora jipya la balestiki lifikalo umbali wa kilomita 700 baharini

Kombora jipya la balestiki la baharini lililoundwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC liitwalo Zulfiqar Basir limezinduliwa leo katika maonyesho ya uwezo wa kistratejia ya vikosi vya anga za mbali vya jeshi hilo.

Maonyesho ya kudumu ya uwezo wa kistratejia ya vikosi vya anga za mbali vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu yamefunguliwa leo hapa mjini Tehran.

Kombora la Zulfiqar Basir ambalo limewekwa kwenye maonyesho hayo kwa mara ya kwanza lina uwezo wa kulenga shabaha chini ya bahari iliyoko umbali wa kilomita 700.

Kabla ya hapo, makombora ya balestiki ya baharini ya Iran ya Ghuba ya Uajemi na Hormuz yalikuwa na uwezo wa kufika umbali wa kilomita 300, lakini kutokana na kuboreshwa uundaji wa aina hiyo ya makombora, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limezindua aina mpya ya kombora la balestiki la baharini la Zulfiqar Basir linalofika umbali wa kilomita 700.

Kombora la Balestiki la baharini la Zulfiqar Basir

Katika maonyesho hayo yanayoakisi mafanikio na uwezo wa kistratejia wa vikosi vya anga za mbali vya IRGC, yamezinduliwa pia mafanikio mengine kadhaa ya ubunifu na uundaji katika nyuga za makombora, ndege zisizo na rubani za droni, satalaiti, mifumo ya ulinzi wa anga ya utambuzi na ugunduzi, vita vya kielektroniki na vilevile mafanikio yaliyopatikana katika vituo vya masuala ya utafiti na uchunguzi.

Katika maonyesho hayo ya kudumu yanayoakisi uwezo wa kistratejia ya vikosi vya anga za mbali vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu zinaonekana pia athari kadhaa za ndege zisizo na rubani za wavamizi, zikiwemo za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo zilitunguliwa na mitambo ya ulinzi wa anga wa vikosi vya anga za ambali vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.../

Tags

Maoni