Sep 28, 2020 12:17 UTC
  • Iran yakadhibisha madai ya kufanya mazungumzo na Marekani nchini Oman

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekanusha vikali taarifa zinazodai kuwa Jamhuri ya Kiislamu imefanya mazungumzo na Marekani huko nchini Oman.

Saeed Khatibzadeh amesema hayo leo Jumatatu hapa mjini Tehran na kubainisha kuwa, Donald Trump hana ufahamu juu masuala ya uhusiano wa kimataifa, na kwamba madai yake juu ya mazungumzo na Iran yametolewa kwa maslahi ya siasa za ndani ya nchi hiyo.

Khatibzadeh amekadhibisha habari hizo za uvumi zilizochapishwa na gazeti la Aljaridah la Kuwait na kueleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijafanya na katu haitafanya mazungumzo na Marekani.

Amesisitiza kuwa, msimamo wa Iran juu ya kufanya mazungumzo na Marekani uko wazi, thabiti, na ulioamuliwa. Amesema iwapo Marekani inataka kurejeshwa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, sharti ikikiri makosa yake, iheshimu sheria za kimataifa, ifute vikwazo vyake vya kidhalimu dhidi ya taifa la Iran, na kisha ifidie hasara zote ilizoisababishia nchi hii kutokana na mashinikizo yake ya kiuchumi.

Trump anadai kuwa anataka kufikia makubaliano na Iran licha ya kuiondoa US katika mapatano ya JCPOA

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Trump anadai kuwa Iran inataka kufikia makubaliano na Marekani katika hali ambayo, mwanasiasa huyo wa Republican anakabiliwa na wakati mgumu hivi sasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba. 

Ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono mwito wa kufanyika mazungumzo ya kieneo uliotolewa na Waziri Mkuu wa Kuwait na kueleza bayana kuwa, Iran daima imekuwa ikipendekeza suala la kufanyika mazungumzo baina ya nchi za eneo la Asia Magharibi, na ndiposa ikaandaa Mpango wa Amani wa Hormuz. 

 

Tags

Maoni