Sep 29, 2020 01:28 UTC
  • Uwezo wa jeshi la majini la Iran, udharura wa kijilinda na kukabiliana na adui

Uwezo wa jeshi la majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika pwani ndefu ya kaskazini na kusini mwa nchi una umuhimu mkubwa katika ngazi ya kikanda na kimataifa.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina mpaka wenye urefu wa karibu kilomita elfu tatu na kwa sababu hiyo inalipa umuhimu mkubwa suala la kulinda mipaka yake ya majini. Usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi unalilazimu jeshi la majini la Jamhuri ya Kiislamu liwe katika utayarifu wa hali ya juu zaidi wa kuweza kulinda nchi mbele ha shambulizi na chochoko za aina zote za maadui. Katika uwanja huo maonesho ya kudumu ya uwezo wa kistratijia wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) yaliyofunguliwa Jumapili iliyopita mjini Tehran yanahesabiwa kuwa sehemu ya matunda na mafanikio ya kijeshi ya Iran katika uwanja huo.

Kombora la Dhulfiqar Basir ambalo limeonyeshwa kwa mara ya kwanza katika maonyesho hayo lina uwezo wa kulenga shabaha baharini umbali wa kilomita mia saba (700). Awali makombora ya balestiki ya Iran ya kulenga shabaha baharini kama kombora la Ghuba ya Uajemi na lile la Hormuz yalikuwa na uwezo wa kupiga shabaha umbali wa kilomita 300. Sasa masafa ya makombora ya baharini ya Iran yameongezeka na kuweza kulenga shabaha umbali wa kilomita 700 baada ya kuzinduliwa kombora la Zulfiqar Basir. 

Kombora la Dhulfiqar la Iran. Uwezo wa kiulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ni furaha kwa marafiki

 

Maonyesho ya kudumu ya mafanikio na uwezo wa kistratijia wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni dhihirisho la matunda ya jeshi hilo katika masuala ya makombora, ndege zisizo na rubani, satalaiti, mitambo ya kurushia makombora, rada za aina mbalimbali na zana za vita vya kielektroniki. 

Meja Jenerali Hossein Salami ambaye ni Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika ufunguzi wa maonyesho hayo kwamba Jamhuri ya Kiislamu haitasimama hata dakika moja katika uzalishaji wa zana za kujilinda na kuongeza kuwa: Sehemu kubwa zaidi ya mafanikio haya ya kustaajabisha yamepatikana katika kipindi cha vikwazo dhidi ya Iran, suala ambalo linabainisha uhakika kwamba, Jamhuri ya Kiislamu imebadilisha vikwazo hivyo na kuwa fursa ya maendeleo katika utengenezaji na uzalishaji wa zana za kujihami.

Wakati huo huo kamanda wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Admeri Alireza Tangsiri amesema, kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini makombora ya vyombo vya majini viliyokuwa vimenunulia kutoka nje ya nchi yalikuwa na uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 45 tu. Admeri Tangsiri ameongeza kuwa: Hii leo na kwa hima na bidii ya vijana wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Wizara ya Ulinzi, makombora ya cruise yanayotengenezwa hapa nchini yana uwezo wa kulenga shabaha umbali wa kilomita 700 hadi elfu moja. 

Lango Bahari la Hormuz

 

Ni vyema kuashiria hapa pia kwamba, kikosi cha kistratijia cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kinadhibiti kikamilifu harakati zote katika Lango Bahari la Hormuz na Ghuba ya Uajemi na kina nafasi muhimu sana katika mlingano wa maeneo ya baharini katika maji ya kikanda na kimataifa. Kwa msingi huo suala la kuimarisha jeshi hilo kwa zana za kisasa kabisa yakiwemo makombora ya kisasa ni jambo la dharura ambalo linazidisha usalama na amani katika eneo la kistratijia la Ghuba ya Uajemi. 

Jarida la Kimarekani la The National Interest limechapisha uchambuzi kuhusu uwezo wa kijeshi na wa kujihami wa Iran katika nyanja mbalimbali na kuandika kuwa: Uwezo wa kijeshi ni uhakika ambao Iran imeamua kuudhihirisha na kuuweka wazi.

Hii leo jeshi la majini la Jamhuri ya Kiislamu limejizatiti kwa meli za kivita zenye kasi kubwa, boti zenye uwezo wa kufyatua makombora, na manowari za kisasa kama ile ya Ghadir.

Vilevile Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lina mamia ya boti za mwendo kasi zenye uwezo wa kubeba makombora ya kisasa zinazoliwezesha jeshi hilo kupigana vita katika mazingira magumu. Vilevile Iran inahesabiwa kuwa miongoni wa nchi kumi zinazoongoza kwa makombora ya ardhi kwa ardhi, makombora ya anga, rada za kisasa, ndege zisizo na rubani (drone) zana za vita vya kielektroniki na sataiti za masuala ya kijeshi.            

Tags

Maoni