Sep 29, 2020 08:19 UTC
  • Madai ya kufanyika mazungumzo kati ya Iran na Marekani; propaganda za matumizi ya ndani ambazo labda zimfae Trump

Gazeti la Al-Jarida linalochapishwa nchini Kuwait limechapisha habari inayodai kuwa Iran na Marekani zimeanza mazungumzo nchini Oman ili kuweza kufikia mapatano mapya kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na hata ziko tayari pia kusaini mkataba wa ushirikiano.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekanusha madai hayo na akaeleza bayana kwamba, hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika baina na Iran na Marekani na kwamba hizo ni propaganda tu kwa ajili ya matumizi ya ndani ya Marekani ambazo labda zinaweza zikamfaa Trump.

Saeed Khatibzadeh alitoa ufafanuzi huo siku ya Jumatatu katika mkutano na waandishi wa habari na akaeleza kwamba Trump hana ufahamu wowote sahihi kuhusu dhati ya mahusiano ya kimataifa na uhusiano wa Iran na Marekani. Khatibzadeh aliongeza kuwa, inambidi Trump akubali makosa yake na kusimamisha vita vya kinyama na vya pande zote pamoja na vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran sambamba na kufidia hasara zote alizolitia taifa la Iran kupitia vita hivyo. Ni baada ya kuyafanya hayo, ndipo huenda akaweza kutengewa kijinafasi ndani ya chumba cha JCPOA.

Saeed Khatibzadeh

Ukweli ni kwamba Marekani haijawahi kufanya lolote lile kwa nia njema ambayo ni kaida na msingi mkuu wa mahusiano ya kimataifa. Kwa hatua yake ya upande mmoja ya kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kurejesha tena vikwazo sambamba na kuwaadhibu wale walioendelea kuheshimu azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani ilihalifu na kukiuka makubaliano hayo ya kimataifa pamoja na azimio hilo la UN. Kutokana na rekodi hiyo ya Washington, na kwa kuzingatia sera za kiuadui za Trump dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, mazungumzo kati ya Iran na Marekani yanaelezeka kama jambo lisilowezekana.

Mwaka mmoja nyuma mnamo tarehe 17 Septemba 2019 wakati Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei alipohutubia katika ufunguzi wa darsa yake ya Fiqhi sambamba na kuanza mwaka mpya wa masomo katika vyuo vya kidini vya hapa nchini, alitanabahisha kuwa, hatua inazochukua Marekani ili kuweza kufanya mazungumzo na Iran ni hila na mbinu ya kutaka kuthibitisha kuwa mashinikizo yake ya kiwango cha juu kabisa yamezaa matunda.

Ayatullah Khamenei alieleza kwamba, mazungumzo na Marekani yanategemea masharti maalumu itakayotekeleza nchi hiyo na akabainisha kuwa, "Endapo Marekani itabadili kauli yake na kujuta kwa iliyoyafanya na ikarejea kwenye makubaliano ya nyuklia iliyoyakiuka, hapo ndipo itaweza kushiriki katika mjumuiko wa nchi wanachama wa makubaliano hayo zinazoshiriki katika mazungumzo na Iran; lakini kinyume na hivyo hakuna mazungumzo yoyote na katika ngazi yoyote, yatakayofanyika baina ya viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu na Wamarekani, si New York wala kwengineko kusiokuwa huko."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei

Ukweli ni kwamba diplomasia ya Marekani si ya muelekeo wa kufanya mazungumzo, bali ni ya siasa za kuhujumu kwa kutumia hila na hadaa. Katika hali ya sasa maji yamemfika shingoni Trump kutokana na kibarua kigumu kinachomkabili cha kampeni za uchaguzi huku akiandamwa na shutuma na malalamiko makubwa ya wananchi na matatizo yanayotokana na maambukizo makubwa ya virusi vya corona yaliyosababishwa na uendeshaji mbovu wa serikali yake. Katika uga wa kikanda na kimataifa na hata katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia, siasa zake za kibabe na za kutaka kuburuza mataifa mengine zimegonga mwamba.

Mohammad Marandi, mtaalamu wa masuala ya Marekani ameaashiria madai yaliyotolewa kuhusu mazungumzo ya siri yanayodaiwa kufanyika kati ya Iran na Marekani nchini Oman na akaeleza kwamba: Marekani ni utawala unaotaka kujivutia kila kitu na wala haufikirii mazungumzo ya kunufaisha kila upande. Trump hana matumaini ya kushinda; na usambazaji wa habari za aina hii unafanyika zaidi kwa ajili ya kampeni za uchaguzi.

Malengo ya Marekani ya kutaka kufanya mazungumzo na Iran yanaweza kubainishwa katika nukta mbili kuu:

Nukta ya kwanza ni kutaka kuthibitisha hoja kwamba Iran imesalimu amri mbele ya utekelezaji wa wakati mmoja wa "vitisho na vikwazo" dhidi yake.

Nukta ya pili ni kutumia wenzo wa kuiburuza Iran kwenye meza ya mazungumzo ili kulitumia hilo kipropaganda kwa ajili ya kumpa itibari Trump kama rais makini na mpenda mazungumzo.

Hata hivyo utambulisho na dhati halisi ya Trump inatambuliwa vyema, si na taifa la Iran pekee bali hata na Wamarekani na dunia nzima. Licha ya siasa zao mbovu wanazotelekeza kuhusiana na Iran, viongozi wa Marekani wangali wanakazania kuendeleza makosa yao ya huko nyuma. Kueneza uvumi wa kufanya mazungumzo na Iran, nao pia ni mwendelezo wa fikra na mawazo hayo potofu.../

Maoni