Oct 14, 2020 02:24 UTC
  • Waziri wa Afya wa Iran: Majaribio ya chanjo wa corona hapa nchini yanaendelea vizuri

Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa majaribio ya chanjo ya virusi vya corona inayotengenezwa hapa nchini yanaendelea vizuri kwa wanyama na kwamba chanjo hiyo itaanza kufanyiwa majaribio kwa wanadamu hivi karibuni.

Daktari Saeed Namaki aliyasema hayo jioni ya jana katika kikao cha maafisa wa wizara hiyo mjini Tehran kilichohudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah).

Namaki amesema kuwa, majaribio ya chanjo hiyo yaliyofanywa kwa kutumia tumbili yamekuwa na matokeo mazuri na katika kipindi cha wiki mbili hadi tatu zijazo chanjo hiyo itaanza kufanyiwa majaribio kwa binadamu. Amesisitiza kuwa awamu zote za majaribio hayo zinafanyika kwa kuzingatia vigezo vya kimataifa.

Waziri wa Afya wa Iran pia ameashiria athari mbaya za vikwazo kwa uchumi wa Iran na kusema kuwa: Vikwazo vya kidhalimu vya Marekani vinakwamisha hata ununuzi wa dawa na vifaa vya tiba.

Iran inafanyia majaribio chanjo ya virusi vya corona

Wakati huo huo Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran amesema kuwa jeshi hilo limetayarisha suhula zake zote kwa ajili ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona hapa nchini.

Meja Jenerali Hussein Salami amesema kuwa uwanja wa kupambana na corona ni mtihani mkubwa ambao umedhihirisha thamani za jamii ya madaktari na wahudumu wa tiba hapa nchini kama kujitolea, uaminifu na uchapakazi.

Kamanda Salami amesisitiza kuwa jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu litaendelea kutumia suhula zake zote kama mahospitali na vituo vyake vya afya kwa ajili ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona.

Tags

Maoni