Oct 18, 2020 08:20 UTC
  • Iran: Leo ni siku muhimu kwa walimwengu baada ya kufikia tamati vikwazo vya silaha dhidi ya Tehran

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa rasmi kwa mnasaba wa siku ya leo ya tarehe 18 Oktoba ya kufikia tamati muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya taifa hili na kueleza kwamba, hii ni siku muhimu kwa jamii ya kimataifa.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, kuanzia leo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaweza kununua silaha yoyote kutoka popote kulingana na mahitaji yake ya kiulinzi kama ambavyo pia inaweza kuuza nje silaha zake inazozalisha kwa mujibu wa sera zake za kiulinzi.

"Leo ni siku muhimu kwa walimwengu, kwani kinyume na njama za utawala wa Marekani, jamii ya kimataifa imesimama kidete na kulilinda azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA)," imeeleza sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Moja ya vipengee muhimu vya mapatano ya nyuklia ya JCPOA ni azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lina kipengee kuhusu kufutwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran miaka mitano baada ya kuanza kutekelezwa mapatano hayo.

 

Aidha taarifa hiyo imeashiria hila na mchezo mchafu wa Marekani katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita ambapo ilifanya kila inaloweza kuhakikisha kwamba, muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran unaongezwa na kubainisha kwamba, Washington inapaswa kuachana na moyo wake wa uharibifu na badala yake iheshimu na kufungamana kikamilifu na maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Viongozi mbalimbali wa Iran wamezungumzia tukio la leo la kufikia tamati muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya taifa hili na kulitaja hili kama ushindi mwingine wa Tehran mbele ya ubeberu wa Marekani.

Tags