Oct 18, 2020 10:08 UTC
  • Kumalizika muda wa vikwazo vya silaha vya Iran; ujumbe na matokeo yake

Baada ya kupita miaka mitano ya utekelezaji wa mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA, hatimae muda wa vikwazo vya silaha vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umemalizika leo Jumapili, Oktoba 18, 2020.

Baada ya kumalizika muda wa vikwazo hivyo, sasa Iran iko huru kuuza na kununua silaha na zana na kivita nje ya nchi. Aidha vikwazo vya kusafiri nje maafisa 23 wa kisheria wa Iran vimeondolewa kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopasisha makubaliano ya JCPOA. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa tamko rasmi kufuatia kumalizika muda wa vikwazo vya silaha vya Iran na kusema:

Leo ni siku muhimu sana kwa jamii ya kimataifa ambapo kinyume kabisa na njama za utawala wa kibeberu wa Marekani, azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mapatano Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) vimeweza kulindwa.

Azimio nambari 2231 lililopasisha mapatano ya kimataifa ya nyuklia, JCPOA

 

Katika kipindi cha miezi kadhaa nyuma, awali Marekani ilijaribu kurefusha muda wa vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran. Hata hivyo muswada wa azimio uliowasilishwa na Washington kwa Baraza la Usalama ulipigwa teke vibaya sana. Katika wanachama 15 wa baraza hilo, ni kijinchi kimoja tu ndicho kilichouunga mkono muswada huo huku wajumbe wengine wakiupinga kikamilifu na wengine wakikataa kuupigia kura. Baada ya kupata pigo hilo, Marekani haikuingia adabu, bali ilifanya njama nyingine za kutaka kurejesha "otomatiki" vikwazo ilivyokuwa imeondolewa Iran baada ya kufikiwa mapatano ya JCPOA. Hata hivyo mara hii Donald Trump na genge lake huko White House walipata pigo kubwa zaidi. Njama hizo hazikufika popote maana Trump alikuwa ameshajitoa kwenye mapatano hayo, hivyo hakuwa na haki yoyote kutumia vipengee vya JCPOA kuirejeshea vikwazo Iran. Leo pia Marekani imepata pigo jingine kubwa zaidi baada ya kumalizika muda wa vikwazo vya silaha vya Iran. Washington ilikuwa na matumaini sana na kuendelea vikwazo hivyo hasa wakati huu ambapo uchaguzi wa rais umebakia siku chache tu kufanyika huko Marekani na Trump yuko katika mazingira mazito ndani na nje ya Marekani. Kumalizika muda wa vikwazo hivyo ni pigo kubwa kwa itibari ya Marekani duniani.

Amma umuhimu wa suala hilo tunaweza kuungalia katika vipembe viwili:

Kipembe cha Kwanza ni upeo wa kisiasa wa suala hilo na udharura wa kuheshimiwa ahadi, maamuzi na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Suala hilo lina ujumbe wa wazi nao ni wa kupinga na kukabiliana kikamilifu na fikra ya Donald Trump ya kukataa ushirikiano na kujikumbizia kila kitu upande wake.

Kazem Gharibabadi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika taasisi za kimataifa zenye makao yao mjini Vienna Austria, mapema leo asubuhi ameliambia shirika la habari la IRNA kwa njia ya simu kwamba: Suala hili lina umuhimu mkubwa kwa sababu vikwazo muhimu zaidi, yaani vikwazo na mashinikizo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika maudhui tofauti vimeondolewa na sasa serikali zote haziwezi kutumia madai ya vikwazo vya Baraza la Usalama katika miamala yao ya silaha na Iran.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesambaratisha njama za Marekani dhidi yake

 

Amma Kipembe cha Pili ni matokeo na taathira za kisheria za kumalizika muda wa vikwazo vya silaha vya Iran. Nukta muhimu sana katika suala hili ni nafasi ya ununuaji silaha katika stratijia ya kiulinzi ya Iran.

Hata katika miaka ya kabla ya kuwekwa vikwazo hivyo, Iran ilikuwa inatenga fedha kidogo tu kununua silaha kutoka nje. Sababu yake ni kwamba stratijia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimsingi imesimama juu ya kutegemea uwezo wa ndani kujidhaminia usalama wake. Katika miaka ya hivi karibuni, Iran imepiga hatua kubwa katika uzalishaji wa zana zinazokubalika kimataifa za kijeshi. Mkakati huo umeendelea muda wote kuwa msingi wa asili wa hatua zote za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kulinda uwezo wake wa kiulinzi. Tab'an Tehran imekuwa ikisisitiza muda wote kwamba haina haja kabisa na silaha zisizokubalika kimataifa wala kujilimbikizia silaha za kuhatarisha usalama wa eneo hili.

Kwa kweli ni kama alivyosema Dk Mohammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwamba: Kumalizika muda wa vikwazo vya silaha vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ni ushindi kwa malengo matukufu ya ushirikiano wa kimataifa na pia kwa usalama na amani ya kikanda na ya kimataifa.