Oct 19, 2020 03:03 UTC
  • Zarif: Iran inaunga mkono mchakato wa amani Afghanistan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono mchakato wa amani nchini Afghanistan ambao unaongozwa na Waafghani wenyewe.

Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliyasema hayo jana Jumapili hapa mjini Tehran wakati alipokutana na Abdullah Abdullah, mkuu wa Baraza Kuu la Maelewano ya Kitaifa la Afghanistan.

Katika kikao hicho, Zarif amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaiunga mkono serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Afghanistan na mchakato wa kutafuta amani nchini humo ambao unaongozwa na Waafghani wenyewe. Aidha amesema Iran inaunga mkono mapatano yatakayofikiwa katika mazungumzo kama hayo.

Waziri Zarif amempongeza Abdullah kwa kushiriki katika mchakato wa kisiasa na kukubali kuongozi Baraza Kuu la Maelewano ya Kitaifa Afghanistan. Aidha amesema Iran inaunga mkono kushirikishwa kundi la Taliban katika muundo wa kisiasa nchini Afghanistan.

Abdullah Abdullah, mkuu wa Baraza Kuu la Maelewano ya Kitaifa nchini Afghanistan

Kabla ya kufika Iran, Abdullah Abdullah pia alitembelea India na Pakistan na ambapo katika nchi zote hizo tatu amewasilisha maeleezo kuhusu mchakato wa kuleta maelewano ya kitaifa kwa ajili ya kurejesha amani na kumaliza vita kikamilifu Afghanistan.

Weledi wa mambo ya kisiasa wanaamini kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi muhimu sana katika mchakato wa amani nchini Afghanistan na kwamba Tehran inaweza kuwa na nafasi muhimu sana katika kuleta amani ya kudumu na utulivu Afghanistan.

Tags

Maoni