Oct 19, 2020 03:06 UTC
  • Nchi nyingi zinataka kununua silaha za Iran

Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, amesema nchi kadhaa zimetangaza kuwa tayari kununua silaha zilizoundwa nchini Iran.

Akizungumza Jumapili, Mojtaba Zonnouri, Mwenyekiti  wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, amesema Iran iko tayari kuuzwa silaha kwa nchi zitakazoomba kuuziwa. Aidha amesema Iran inaweza kukidhi mahitaji yake ya fedha za kigeni kwa kuuza silaha.

Zonnouri amesema vikwazo vimeiwezesha Iran kuimarisha uwezo wake wa kuunda silaha na zana za kujihami kwa kutegemea wataalamu wa ndani ya nchi.

Baada ya kupita miaka mitano ya utekelezaji wa mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA, hatimae muda wa vikwazo vya silaha vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulimalizika jana Jumapili, Oktoba 18, 2020.

Ndege ya kivita aina ya Kauthar (Kosar) iliyoundwa Iran

Baada ya kumalizika muda wa vikwazo hivyo, sasa Iran iko huru kuuza na kununua silaha na zana na kivita nje ya nchi. Aidha vikwazo vya kusafiri nje maafisa 23 wa kisheria wa Iran vimeondolewa kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopasisha makubaliano ya JCPOA. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran jana ilitoa tamko rasmi kufuatia kumalizika muda wa vikwazo vya silaha vya Iran na kusema:

Leo ni siku muhimu sana kwa jamii ya kimataifa ambapo kinyume kabisa na njama za utawala wa kibeberu wa Marekani, azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mapatano ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) vimeweza kulindwa.