Oct 19, 2020 10:04 UTC
  • Sisitizo la Iran la kuunga mkono mchakato wa amani na kurejeshwa uthabiti nchini Afghanistan

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imeonyesha katika sera zake za kigeni kwamba, inaunga mkono uthabiti wa kisiasa, amani na utulivu nchini Afghanistan, na utendaji huu siku zote umekuuwa ukipewa kipaumbele katika sera za kigeni za Tehran.

Kwa maneno mengine yenye umakini zaidi inapasa kusema kuwa, Afghanistan iliyojengeka vyema, huru, yenye ustawi na ambayo ina amani na uthabiti daima limekuwa takwa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana Jumapili alikutana na kufanya mazungumzo hapa mjini Tehran na Abdullah Abdullah, Mkuu wa Baraza Kuu la Maelewano ya Kitaifa la Afghanistan ambapo kwa mara nyingine tena alisisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaiunga mkono serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Afghanistan na mchakato wa kutafuta amani nchini humo ambao unaongozwa na Waafghani wenyewe, kama ambavyo inaunga mkono mapatano yatakayofikiwa katika mazungumzo kama hayo.

Abdullah Abdullah, Mkuu wa Baraza Kuu la Maelewano ya Kitaifa la Afghanistan katika mazungumzo yake na Rais Hassan Rouhani

 

Waziri Zarif amempongeza Abdullah Abdullah kwa kushiriki katika mchakato wa kisiasa na kukubali kuwa Kiongozi wa Baraza Kuu la Maelewano ya Kitaifa Afghanistan na akasema kuwa, Iran inaunga mkono kushirikishwa kundi la wanamgambo wa Taliban katika muundo wa kisiasa nchini Afghanistan.

Abdullah Abdullah ambaye jana aliwasili hapa mjini Tehran kwa safari ya siku tatu lengo likiwa ni kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu hapa nchini, kabla ya kuja hapa nchini alizitembelea nchi za India na Pakistan na ambapo katika nchi zote hizo amewasilisha maelezo kuhusu mchakato wa kuleta maelewano ya kitaifa kwa ajili ya kurejesha amani na kumaliza vita kikamilifu nchini Afghanistan.

Nafasi na mchango wa Iran kieneo hususan katika uga wa siasa za kigeni za Afghanistan daima umekuwa ukipongezwa na Rais wa Afghanistan pamoja na viongozi wengine waandamizi wa serikali ya Kabul na kuutaja kuwa muhimu na wenye taathira chanya.

Mazungumzo ya Spika wa Bunge la Iran Muhammad Baqir Qalibaf na Abdullah Abdullah, Mkuu wa Baraza Kuu la Maelewano ya Kitaifa la Afghanistan

 

Ni kwa msingi huo ndio maana viongozi waaandamizi wa Afghanistan daima wamekuwa wakikaribisha kwa mikono miwili ushiriki wa Tehran katika mipango na ubunifu wa amani nchini Afghanistan.

Katika uwanja huo na katika mazungumzo yake na Muhammad Baqir Qalibaf, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Abdullah Abdullah, Mkuu wa Baraza Kuu la Maelewano ya Kitaifa la Afghanistan sambamba na kusifu na kuthamini himaya na uungaji mkono wa Iran kwa nchi yake alisema: Lengo la Tehran ni kuunga mkono amani chini ya kivuli cha Jamhuri ya Kiislamu ya Afghanistan na katiba ya nchi hiyo na daima Iran katika miongo minne ya hivi karibuni imekuwa pamoja na bega kwa bega na wananchi wa Afghanistan.

Kuhusiana na mahusiano ya Iran na Afghanistan kuna nukta mbili ambazo ni muhimu kuzitaja.

Nukta ya kwanza; umuhimu wa uhusiano wa Iran na Afghanistan unatokana na nchi mbili hizi kuwa majirani na kuwa na mpaka wa pamoja. Kuwa jirani Iran na Afghanistan kumekuwa kukipelekea matukio chanya au hasi ya Afghanistan kuwa na taathira kwa Iran.

Nukta ya pili; ni nafasi chanya na yenye kujenga ya Iran katika kipindi cha miongo minne iliyopita ambapo taifa hili limeiunga mkono Afghanistran bila ya kuwa na tamaa ya kupata kitu mbadala.

Abdullah Abdullah, alipowasili jana Jumapili (18.10.2020) mjini Tehran kwa safari ya siku tatu

 

Akizungumza hivi karibuni kwa njia ya simu na Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisisitiza kuwa, tunalitambua suala la kustawisha amani na uthabiti nchini Afghanistan kuwa ni katika fremu ya kustawishwa amani na uthabiti wetu; na tunaamini kwanmba, hitilafu zilizopo baina ya mirengo na makundi ya Afghanistan zinaweza kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo na daima tupo pamoja na serikali na wananchi wa nchi hiyo katika njia hii.

Kile ambacho kiko wazi ni kwamba, amani, uthabiti na ustawi wa Afghanistan ni kwa maslahi ya Iran na mataifa yote ya eneo. Kadiri Afghanistan inavyokuwa ina nguvu, imara na thabiti, ndivyo pia uhusiano wa nchi hiyo na mataifa jirani unavyokuuwa imara na madhubuti.

Kwa muktadha huo, safari ya Abdullah Abdullah, Mkuu wa Baraza Kuu la Maelewano ya Kitaifa la Afghanistan na ujumbe alioandamana nao hapa mjini Tehran ni fursa muhimu ya viongozi wa pande mbili ambapo sambamba na kufanya mazungumzo kuhusiana na mwenendo wa amani nchini Afghanistan waweze pia kujadiliana mambo yanayohusiana na uhusiano wa pande mbili na maudhui nyingine ambazo Tehran na Kabul zina mitazamo ya pamoja kuhusiana nazo.