Oct 19, 2020 15:27 UTC
  • Sayyid Ibrahim Raisi
    Sayyid Ibrahim Raisi

Mkuu wa Idara ya Mahakama nchini Iran amezitahadharisha nchi za Magharibi kuhusu suala la kuwapa hifadhi mafisadi wa kiuchumi na kusema mafisadi hao wasidhani kuwa, fedha wanazoiba zitawafaidisha.

Sayyid Ibrahim Raisi ambaye mapema leo alikuwa akihutubia kikao cha Baraza Kuu la Maafisa wa Idara ya Vyombo vya Mahakama amelipongeza Jeshi la Polisi na Polisi ya Kimataifa (Interpol) kwa kumrejesha nchini Iran mmoja kati ya watuhumiwa wa kesi za ufisadi wa kifedha kutoka Uhispania na akasema: Wale wanaodhani kuwa, wanaweza kufanya uhalifu na kukwepa sheria kwa kutorokea nje ya nchi wamo katika makosa.

Raisi ameongeza kuwa, Idara ya Vyombo vya Mahakama ya Iran haitawapa amani hata kidogo wale wanaopora mali ya umma na itaendelea kufuatilia kwa nguvu zote suala la kuwarejesha nchini watuhumiwa wote wa ufisadi na wale waliopora mali ya taifa. 

Sayyid Ibrahim Raisi

Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran amezitaka tawala za Magharibi zisiruhusu nchi hizo kuwa makimbilio salama ya waporaji wa mali ya umma na mafisadi wa kiuchumi.

Sayyid Ibrahim Raisi ameashiria pia suala la kumalizika muda wa vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran na kusema kuwa: Hatupasi kutosheka na suala la kushindwa kisiasa Marekani katika kadhia hii bali kuna ulazima wa kuchukua hatua zaidi za kuhakikisha vikwazo vya kidhalimu vya serikali ya Washington na nchi za Magharibi kwa ujumla vinaondolewa.