Oct 19, 2020 15:37 UTC
  • Corona yaendelea kuua watu katika wimbi jipya la maambukizi, mamia ya Wairani waaga dunia katika siku moja

Wimbi jipya la maambukizi ya virusi vya corona linaendelea kuchukua roho za watu katika maeneo mbalimbali ya dunia na kuathiri uchumi na ustawi katika nchi mbalimbali.

Wizara ya Afya ya Iran leo imetangaza kuwa, zaidi ya watu elfu nne wamepatwa na virsi vya corona hapa nchini katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita.

Msemaji wa Wizara ya Afya ya Iran, Daktari Sima Sadat Lari amesema kuwa, katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita Wairani 4,251 wamepatwa virusi vya corona na kwamba 948 miongoni wamelazwa mahospitalini. Daktari Lari ameongeza kuwa wagonjwa 337 wa ugonjwa wa COVID-19 wameaga dunia hapa nchini katika masaa 24 yaliyopita.

Msemaji wa Wizara ya Afya ya Iran amongeza kuwa hadi sasa wagonjwa 4,31,360 wa corona wamepona na kuruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kupewa matibabu. 

Sadat Lari

Wakati huo huo takwimu za kimataifa zinasema kuwa zaidi ya watu milioni arubaini laki 3 na sabini elfu wamepatwa na virusi vya corona katika nchi mbalimbali za dunia na milioni moja laki moja na kumi na tisa elfu 544 (1,119,544) miongoni mwao wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo. 

Marekani bado inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya maambukizi ya corona kwa kuwa na zaidi ya wagonjwa milioni nane laki tatu wa COVID-19 na vifo vya zaidi ya watu laki mbili na 25 elfu. India inafuata ikiwa na zaidi ya wagonjwa milioni saba na nusu na Brazil inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na wagonjwa zaidi ya milioni tano wa corona.