Oct 21, 2020 12:51 UTC
  • Iran: OIC itekeleza majukumu yake kukabiliana na wanaoanzisha uhusiano na Israel

Mkuu wa Shirika la Utamaduni na Uhusiano wa Kiislamu Iran (ICRO) amesema, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) inapaswa kutekeleza majukumu yake kuhusiana na Fatuwa ambayo imetolewa na wanazuoni wa Kiislamu kuhusu marufuku ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mkurugenzi wa ICRO Dkt. Abuzar Ebrahimi Turkman ameyasema hayo Jumanne alipohutubia katika kikao cha ushauri cha nchi wanachama wa OIC ambacho kiliandaliwa na Idara ya Masuala ya Kidini Uturuki.

Katika hotuba yake hiyo, Turkman ameashiria hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema kuwa, wanazuoni wa Kiislamu wamepiga marufuku hatua hiyo. Aidha amesema, hii leo ulimwengu wa Kiislamu unahitaji umoja na mshikamano zaidi ya wakati wowote ule.

Ameongeza kuwa, ulimwengu wa Kiislamu unakabiliana na changamoto nyingi kama vile ujinga, migawanyiko, ghasia, misimamo ya kufurutu ada, kukaliwa kwa mabavu ardhi, mauaji, uporaji na masaibu mengine ya watu wa kawaida na wanaodhulumiwa; na yote hayo yanafanyika kwa kisingizio cha Uislamu katika hali ambayo tunafahamu kuwa Uislamu haungi mkono mambo kama hayo.

Ameendelea kusema kuwa, magaidi wakufurishaji wanaungwa mkono na Uistikbari wa kimataifa unaoongozwa na Marekani na Wazayuni kwa lengo la kuharibu taswira ya Uislamu na kupotosha mafundisho ya Kiislamu.

Ebrahimi Turkaman amesema, kunyamazia kimya jinai kama hizo ni sawa na kushirikiana na madhalimu na ameongeza kuwa, madola ya Kiistikbari yanajaribu kueneza chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu na chuki dhidi ya Iran.

Mkuu wa  Shirika la Utamaduni na Uhusiano wa Kiislamu Iran amesema kadhia ya Palestina inapaswa kutatuliwa kwa kufuata pendekezo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Pendekezo hilo linahusu kurejea Wapalestina wote wote katika ardhi zao za jadi na kisha kuitishwe uchaguzi utakaowajumuisha Wapalestina wote asili wakiwemo Waislamu, Wakristo na Mayahudi na baada ya hapo kuundwe mfumo wa kisiasa baada ya kura ya maoni.

Aidha amesema Iran iko tayari kushirikiana kikamilifu na OIC ili kufanikisha uundwaji wa jamii ya Kiislamu iliyostawi.

Tags

Maoni